IMG_9444
Mhandisi Dk. Ezekial Mganilwa, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji  (aliyesimama ) akimualia mgeni rasmi  Mheshimiwa Saidi Mtanda, Mbunge wa Jimbo la  Mchinga  (aliyevaa shati nyeupe) kufungua mafunzo ya usalama barabarani.
EA1B1497
Mhandisi Dk. Ezekial Mganilwa, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji  akimpa mkono Mkuu wa masuala ya Sera na Ushirika wa kampuni ya BG Tanzania, Fred Kiboya.
EA1B1532
Mhandisi Dk. Ezekiel Mganilwa, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji  akimpa mkono Mkuu wa masuala ya Sera na Ushirika wa kampuni ya BG Tanzania, Fred Kiboya.
UZINDUZI wa kampeni ya  usalama barabarani unaofadhiliwa na  BG Tanzania  katika mkoa wa Lindi, kusini mwa  Tanzania wazinduliwa rasmi leo. Baada ya kupewa kazi  ya kufanya utafiti kuhusu ajali za barabarani na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kampuni hiyo ya gesi  ilibaini fursa za kushirikiana katika kuimarisha maadili ya usalama barabarani miongoni mwa wakazi wa Lindi .
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kilibaini visababishi vinne vya mara kwa mara vya ajali za barabani mkoani Lindi ambavyo ni:waendesha pikipiki wasiozingatia maadili ya uendeshaji; mwendo kasi wa waendesha pikipiki;kuendesha huku umelewa; na ukosefu wa alama au ishara za barabarani.  BG Tanzania imeazimia kupunguza kiwango cha ajali kwa kufadhili utoaji wa mafunzo ya usalama barabarani.Hii inaenda sambamba na juhudi za mkoa katika kupunguza ajali za barabarani.
Mkuu wa masuala ya Sera na Ushirika wa kampuni ya BG Tanzania, Fred Kiboya, alihudhuria kwenye sherehe na alisema  “Hili ni tukio muhimu kwa  BG Tanzania.  Kama kampuni tunaamini katika usalama, na tunataka kuhakikisha kuwa, uwepo wetu kusini mwa Tanzania unajenga jamii salama na zenye mafanikio zaidi.Tunaendesha programu ya aina hii Mtwara Mjini, ambapo waendesha pikipiki 600 wanapatiwa mafunzo, na sasa tunarudia zoezi mkoani Lindi.”
Mkoani Lindi, waendesha pikipiki mia mbili watanufaika katika awamu ya kwanza ya programu hii. Kila mmoja atapewa mafunzo ya zaidi ya siku kumi ambapo siku sita zitakuwa kwa ajili ya mafunzo ya nadharia na siku nne zitakuwa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.  Hii itajumuisha utambuzi wa alama na ishara za barabarani, nadharia za uendeshaji wa kujihami,uendeshaji unaofaa, mkao sahihi katika uendeshaji na udhibiti.  Baada ya kumaliza mafunzo kwa ukamilifu, washiriki watapewa cheti cha umahiri katika uelewa wa usalama barabarani pamoja na leseni ya uendeshaji. Kundi la washiriki limechukuliwa kutoka katika kata za  mchinga, Kitomanga, Rutamba, Nyangao na Milola.
Gharama za mafunzo ni Sh. 220,000/-kwa kila mshiriki,hii ikimaanisha kwamba ,kwa ujumla, BG Tanzania imewekeza Shilingi 44,000,000/- kwa ajili ya mafunzo na upatikanaji wa leseni katika awamu hii. Awamu ya pili,ambayo itajumuisha waendesha pikipiki wengine  200 itapangwa baadaye.
Mgeni rasmi kwenye tukio alikuwa Mheshimiwa Saidi Mtanda, Mbunge wa Jimbo la  Mchinga ambapo Mhandisi Dk. Ezekial Mganilwa, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji  aliiwakilisha taasisi yake. Bwana Machumu Leonard, Afisa wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Lindi alihudhuria akiiwakilisha Ofisi ya Kamishina wa Polisi wa Mkoa pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Mwakanjiga.