Kesi ya Ponda: Serikali yakwepa gharama

Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda, jana ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro bila mshitakiwa kuwako mahakamani, hali iliyoibua hisia kuwa serikali imekwepa gharama za kumsafirisha mtuhumiwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kurejea kama ilivyofanya mara mbili.
Ponda wakati anasomewa mashitaka yake kwa mara ya kwanza mahakamani hapa Agosti 18, mwaka huu alisafirishwa kwa helikopta ya polisi na kurejeshwa Dar es Salaam, huku viunga vya mji wa Morogoro vikiwa vimetanda polisi waliojihami kupambana na ghasia.





Agosti 28, mwaka huu, serikali pia iliingia katika gharama kwa mara ya pili kwa kumsafirisha Sheikh Ponda kwenda mahakamani mjini Morogoro kwa kutumia basi la Jeshi la Magereza kutoka jijiji Dar es Salaam ambako anashikiliwa katika gereza la Segerea kwa ajili ya kesi hiyo na kumrejesha tena Dar es Salaam.
Jana kesi hiyo baada ya kutajwa bila Sheikh Ponda kuwapo mahakamani iliahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, itakapotajwa tena.
Sheikh Ponda anashitakiwa kwa uchochezi, kuharibu imani za watu wengine na kushawishi kutendeka kwa kosa.
Wakati kesi hiyo ikitajwa na Mwanasheria wa Serikali, Gloria Rwakibarila, mbele ya Hakimu Agnes Ringo, na kuahirishwa hadi Jumanne ijayo, mahakama hiyo itakapotoa uamuzi wa kumpa dhamana au la, baadhi ya wafuasi wa Sheikh Ponda waliokuwa nje ya uzio wa mahakama walikuwa hawajui kilichokuwa kikiendelea dhidi ya kiongozi wao kwa kuwa ilifanyikia katika chemba.
Hali hiyo ilimlazimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, kutoka nje ya ofisi yake na kwenda kuwaeleza wafuasi hao sababu za kutofikishwa kwa kiongozi wao huyo mahakamani hapo jana.
Hakimu Kabate aliwaambia kuwa kesi hiyo haikutajwa katika mahakama ya wazi kwa sababu ilikuwa inatumika kuendesha vikao vya Mahakama Kuu.
Aliwataka wafuasi hao kuondoka mahakamani hapo mpaka wiki ijayo kiongozi wao atakapofikishwa mahakamani kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana yake.
Baada ya Hakimu huyo kutoa ufafanuzi huo, wafuasi hao walitawanyika kwenye viwanja vya mahakama.
Waandishi wa habari walipomuuliza hakimu huyo sababu za Sheikh Ponda kutofikishwa mahakamani kusikiliza kesi yake ikitajwa, alisema hakukuwapo na umuhimu wa kuwapo mahakamani kwa kuwa ilikuwa ni kwa ajili ya kutajwa tu. Hata hivyo, Hakimu Kabate alisema kuwa mshitakiwa huyo atalazimika kuwapo mahakamani Jumanne ijayo kesi hiyo itakapoitishwa kwa ajili ya kuamua hatma yake ya dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Ponda anayetetewa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Juma Nassoro, anadaiwa kutenda makosa hayo Agosti 10, mwaka huu jioni eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na mawakili wake wamewasilisha ombi  la dhamana na mahakama itatoa maamuzi   Jumanne ijayo  baada ya kupitia vifungu vya sheria.
NIPASHE jana lilipomuuliza Wakili Nassoro sababu za kutokwenda Morogoro wakati kesi ya mteja wake ikitajwa, alisema kuwa jana ilienda kwa ajili ya kutajwa kwa hiyo hakukuwa na umuhimu sana wa kwenda mahakamani.
Hata hivyo, aliongeza kuwa hajui sababu ya Sheikh Ponda kutopelekwa mahakamani pengine kwa sababu ilikuwa kwa ajili ya kutajwa.
SOURCE: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم