SALAAM ZA PONGEZI KUTOKA HISIA ZA MWANANCHI
Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa mwana habari mwenzetu ndugu Issa Michuzi na Blog yake
www.issamichuzi.blogspot.com kwa kazi kubwa walioifanya na wanayoendelea
kuifanya ya kuhabarisha jamii yetu kwa muda wa Miaka tisa (9) mfululizo
bila kupumzika.
Blog ya Issa Michuzi imetimiza miaka 9 tangu kuanzishwa tarehe 8 Septemba 2005 jijini Helsinki, Finland.
Kwanza kabisa; tunampa hongera Ndugu Michuzi kwa kuandika historia kwa
kuleta mapinduzi ya habari ndani nchini na nje ya Tanzania.
Pili; tumefurahishwa sana kwa kitendo cha Ndugu Michuzi kurudisha
shukrani na fadhila kwa Baba wa Ma-blog Bwana Ndesanjo Macha kwa
kumtambulisha, kumuingiza na kumfungulia blog ya jamii ya
www.issamichuzi.blogspot.com mnamo tarehe 8 Septemba 2005 jijini
Helsinki, Finland.
Tatu; Pongezi za kipekee zimuendee Ndugu Issa Michuzi kwa kazi kubwa ya
kutuhabarisha usiku na mchana pamoja na majukumu yake ya kikazi
akilitumikia vyema Taifa letu la Tanzania katika Ofisi Kuu kuliko zote
akiwa kama Mwanahabari Mpiga Picha (Photo Journalist) mwajiriwa wa
Serikali akifanya kazi chini ya Kurugenzi ya Mawasiliano, Ofisi ya Rais
Ikulu ya Tanzania.
Nne; Ni ukweli usiopingika kwamba Issa Michuzi ni mtu wa watu, anapenda
watu na ucheshi wake umemletea mafanikio makubwa katika tasnia ya
habari. Kwa upande mwingine Michuzi ameitumia vyema nafasi ya kipekee
aliyopata kutuhabarisha kwa kutujuza mambo mbalimbali yanayoendelea
ndani na nje ya nchi. Hakuna ubishi tukijiuliza swali ni wafanyakazi
wangapi waliopo sasa hivi Serikalini katika nafasi kama ya Michuzi, ama
waliopita ambao wamefanya mapinduzi ya habari kama Michuzi?
Ndugu msomaji, ukweli unabaki palepale Michuzi anastahili pongezi za kipekee kwa kuthubutu.
Mwisho kwa kumalizia napenda kuufahamisha Umma kwamba Bwana Issa
Michuzi amekuwa mfano wa kuigwa na jitihada zake na mazingira yake
kikazi yamekuwa chanzo cha mafanikio na umaarufu mkubwa aliojizolea na
kujijengea jina nchini na nje ya nchi. Hongera kwa jitihada na harakati
zako.
Tunatambua pia kwa nafasi uliyonayo kikazi inakupa mlango wa kupata
habari kabla ya vyombo vingine vya habari kupata, na vilevile kwa kuwa
mwajiriwa wa Serikali umejijengea heshima kwa taasisi, wizara na vyombo
vingine vya Kiserikali kukuleletea habari zao moja kwa moja wewe kwanza
kabla ya vyombo vingine, kitu ambacho kimefanya watu wengi tuwe tunasoma
blog yako na kuipenda kitu ambacho ni kuzuri na cha kuigwa.
Post a Comment