Diamond Platnumz |
Tupo
kwenye robo ya tatu ya mwaka 2013. Mwaka huu muziki wa Tanzania
umeendelea kuonesha mapinduzi makubwa kuanzia uwepo wa show nyingi,
malipo makubwa kwa wasanii, wasanii kuwekeza zaidi kwenye video nzuri na
za gharama na thamani yao kuongezeka zaidi.
Ni wakati huu ambapo show za Serengeti Fiesta zinaendelea sambamba na
Kili Music Tour. Kwa kuzingatia idadi ya show wanazofanya, nyimbo zao
zinavyochezwa redioni, utambuzi wa kimataifa (international recognition)
na namna wanavyopenya zaidi kimataifa hii ni list ya wasanii 10 walio
hot zaidi mpaka wakati huu wa robo tatu ya mwaka.
Hakuna ubishi kwamba Diamond Platnumz ndiye msanii wa Tanzania aliye
hot zaidi muda huu. Mwaka 2013 aliuanza vizuri mno licha ya kutokuwa na
wimbo wowote mpya na rasmi zaidi ya Muziki Gani alioshirikishwa tu na
Nay wa Mitego, Kesho uliotoka mwaka jana na Ukimwona na Mapenzi Basi
ambazo si nyimbo alizoziachia rasmi, Diamond ameendelea kusikika kila
kona ya nchini na kwingine na nyimbo zake zikipata rotation ya kutosha
kwenye radio zote, kubwa na ndogo. Mwaka huu ameongoza kwa kufanya show
nyingi kubwa ndani na nje ya nchi.
Kwa makadirio ya haraka, show alizofanya kuanzia Burundi na Congo,
Kenya, Comoro na zile za Tanzania, tangu mwaka uanze hakuna shaka msanii
huyo ambaye Bongo5 imempa jina ‘Bongo Flava Prince’ ameshaweka benki si
chini ya shilingi milioni 500.
Siku chache zilizopita, ameongeza zaidi kasi yake kwa kuachia video
kali ya wimbo wake Number 1, huku akitambulisha mtindo mpya wa uchezaji
alioupa jina ‘Ngololo’. Kwa spidi aliyonayo, itachukua muda mrefu sana,
Diamond kupokonywa kijiti chake cha nafasi ya kwanza alichokishikilia.
Lady Jaydee
Vuguvugu la Anaconda limemrudisha rasmi kwenye chart mwanadada huyu
mkongwe. Licha ya kulianzisha vuguvugu hili kwa matusi, mashambulizi na
madongo mazito dhidi ya wapinzani wake wakubwa, Clouds FM, Lady Jaydee
alijikuta akiungwa mkono na watu wengi na kupandishwa juu kutoka chini
alikokuwa amekaribia kupotea.
Uhai wake ulirejea rasmi baada ya show yake ya miaka 13 kwenye muziki
kwa kufanya show iliyomuingiza mpunga wa kutosha. Mwaka huu amefanikiwa
kuwa na hits mbili namba moja, Joto Hasira na Yahaya. Kwa wiki sita
mfululizo, Yahaya imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwenye Marimba
Music Chart, MMC na bado haoneshi dalili za kupunguza kasi.
Hadi sasa, Lady Jaydee ndiye msanii wa kike anayepata mashavu zaidi kuliko mwingine yeyote.
Ommy Dimpoz
Wengi hawajui ukweli huu, kwamba baada ya Diamond, huenda Ommy Dimpoz
akawa msanii anayelipwa fedha nyingi zaidi kwa sasa. Tangu mwishoni mwa
mwaka jana alipoachia single yake iliyompa tuzo, Me and You
aliyomshirikisha Vanessa Mdee, Ommy amekuwa ni mtu wa show zisizokauka.
Mwaka huu aliongoza kwa kuwa na nominations nyingi zaidi kwenye KTMA
na kuibuka na tuzo tatu. Kama ilivyo kwa Diamond, Ommy ni msanii
anayechaji fedha nyingi zaidi kwa show sasa hivi kiasi kilichomfanya
azikatae shilingi milioni 8 alizoombwa alipwe na kampuni ya Global
Publishers kwenye tamasha la Matumaini.
Hivi karibuni aliandaa show yake mwenyewe nchini Burundi
iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa, ameendelea kuwa mmoja wasanii kwenye
show za Fiesta mwaka huu na hivi karibuni, akiwa na single mpya, Tupogo,
ataanza ziara yake nchini Marekani.
AY
Kwa muda mrefu, AY ameendelea kuimarisha mizizi yake kimataifa na
hadi sasa, hakuna msanii wa Tanzania mwenye mafanikio makubwa kimataifa
kama yeye. Akiwa na tuzo ya CHOMVA 2012 mkononi aliyoipata kutokana na
video ya wimbo wake, I don’t Wanna Be Alone, wiki iliyopita AY alikuwa
msanii pekee wa Tanzania kutaja tena kuwania tuzo hizo zinazojulikana
sasa hivi kama CHOAMVA katika vipengele viwili.
Mwaka huu ameachia ngoma mbili pekee, Jipe Shavu aliyomshirikisha Fid
Q na Bila Kukunja Goti aliyoifanya na swahiba wake Mwana FA na
kumshirikisha Mnaijeria, J-Martins. Hivi karibuni yeye na Mwana FA
wameshoot video ya Bila Kukunja Goti nchini Afrika Kusini na hakuna
shaka kuwa ikitoka itachezwa kwenye vituo vikubwa vya runinga.
Pamoja na jitihada hizo AY, imekuwa ngumu kwake kutajwa kwenye tuzo
za KTMA hali iliyomfanya Mwana FA aandike: “Back to the drawing
board,hii wimbo imeshinda huku,si ‘kill music awards’ waliigomea,kuwa
haikuwa inafaa hata kuwa kwenye nominations zao. Ina maana viwango vyao
ni vya juu hivyo?kuwa unaweza shinda channel O vya kwao ukawa
hujavifikia?ama kubana kwao kwa kipuuzi kumeumbuliwa? I’m not mad..what
my boy @AyTanzania won is much much bigger than ‘KILL music awards’..I’m
just concerned…that was ALL.”
Mwana FA
Mwaka huu Hamis Mwinjuma aliandika historia baada ya kufanya show ya
hip hip kwenye ‘corporate audience. Ikipewa jina, The Finest, Mwana FA
alisindikizwa na bendi kongwe ya Kilimanjaro aka Njenje kuangusha show
iliyofanikiwa sana.
Uhusiano wake na Njenje ulizalisha wimbo wake Kama Zamani ambao
tayari video yake imeendelea kufanya vizuri na pia kuchezwa Channel O.
Mwaka huu Mwana FA alikuwa msanii wa tatu miongoni mwa wasanii wa
Tanzania wanaoingiza fedha nyingi kwenye miito ya simu, nyuma ya Rose
Mhando na Diamond kwa kuingiza shilingi milioni 18.
Mafanikio yake mengine yana uhusiano wa moja kwa moja na yale ya AY
kwa ushirikiano wao wa siku nyingi na hivi karibuni wote walienda nchini
Kenya kutengeneza nyimbo mbili na producer mkongwe, Eric Musyoka wa
Decimal Records.
Chege na Temba
Ni ngumu kuyasema mafanikio ya Chege bila kumtaja Temba na vice
versa. Kwa muda mrefu, wakali hawa wameendelea kuwa pamoja na hivi
karibuni kwenye show za Fiesta wameendelea kutajwa kuwa wasanii
wanaoshangiliwa zaidi kwa kufanya show nzuri kuliko wengine.
Nay wa Mitego
Mwaka huu umekuwa mzuri kwa Nay wa Mitego hasa kwakuwa amekuwa
akipiga show nyingi zinazomuingizia mkwanja mzuri. Nay wa Mitego amehit
zaidi na Muziki Gani aliomshirikisha, Diamond Platnumz. Wimbo huo
ulimsaidia kumfungulia zaidi milango ya neema rapper huyo controversial.
Baada ya kuachia wimbo wake mpya, Salam Zao, Nay alirejea tena kwenye
midomo ya watu, blogs, magazeti na kwenye vituo vya redio na TV
kuhusiana na yale aliyoyasema kwenye wimbo huo. Lakini kama usemi
usemavyo, promotion yoyote ile ni promotion nzuri, aina hiyo ya uimbaji
imeendelea kumweka pazuri.
Ben Pol
Ben alijikuta mahali pazuri zaidi baada ya mwaka huu baada ya
kushinda kipengele cha mtunzi bora wa mashairi ya Bongo Flava kwenye
KTMA. Na baada ya kuachia video yake ya Jikubali, Ben Pol ameendelea
kupanda juu kwa spidi huku akiwa msanii anayetafutwa zaidi kwaajili ya
chorus.
Stamina na Young Killer
Jana na Leo, imewaweka karibu zaidi rappers hawa japokuwa kila mmoja
ana nyimbo zake zinazofanya vizuri. Mwaka huu Young Killer aliuingia na
wimbo wake Dear Gambe ambao laiti kama angekuwa na umri juu ya miaka 18,
angechukua tuzo kibao za KTMA. Wimbo wake mpya sasa ni Mrs Superstar
ambao umezidi kupigia mstari uwezo wake kimashairi. Kwake Stamina naye,
Wazo la Leo aliomshirikisha Fid Q na Mwambie Mwenzio aliomshirikisha
Warda na Darassa zimemweka pazuri na kujikuta yeye na Young Killer
wakiwepo kwenye show zote za Fiesta zinazoendelea.
Madee
Single moja tu, Sio Mimi, imemuingizia Madee zaidi ya shilingi
milioni 130, na kuthibitisha kuwa, hit moja tu inaweza kubadilisha
maisha ya msanii. Hadi leo jina la Madee halikosekani kwenye show nyingi
kubwa na huku akiwa miongoni mwa wasanii wanaonekana kupata shavu la
kufanya show nyingi zaidi za Fiesta mwaka huu.
إرسال تعليق