Ubalozi wa Tanzania Washington DC, wathibitisha marehemu Adubo M.Omer hakuwa Raia wa Tanzania.

Adubo Mustafa Omer Enzi ya uhai wake
Baada ya uchunguzi wa zaidi ya wiki tatu,Ubalozi wa Tanzania Washington DC umethibitisha kuwa Marehemu Adubo M. Omer hakuwa Raia wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania bali alikuwa Raia wa Sudan.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu Dar Es Salaam ilielezwa kuwa,hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa, Marehemu Adubo aliwahi kupewa Uraia wala Pasipoti ya Tanzania.

Aidha,kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa kutoka kwenye taasisi mbali mbali za Kiserikali zilizopo mjini Dallas Texas, Marehemu Adubo M Omer alizaliwa tarehe 25.04.1956 katika sehemu iitwayo Maridi Abang, iliyopo Sudani ya Kusini.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa marehemu Adubo, alikuwa amepewa hati ya kudumu ya ukaazi Nchini Marekani (Permanent Resident card) ambayo ilikuwa inamaliza muda wake tarehe 8.03.2014.

Ubalozi ulipotaka kujua, ilikuwaje hadi ofisi ya 'Medical Examiner' ambayo inafanya uchunguzi wa sababu za kifo cha Marehemu Adubo imtambulishe ubalozini marehemu huyo kama Raia wa Tanzania? Msemaji wa ofisi hiyo alieleza kuwa, hii ni kwa mujibu wa maelezo ambayo marehemu mwenyewe aliyatoa kwenye kituo cha Police cha Dallas, alikokuwa amekamatwa na kuwekwa ndani kwa siku chache kisha akaachiwa kabla ya kifo chake.

Inaelekea Marehemu Adubo hakutaka Uraia wake ujulikane kwa sababu ambazo hazikuweza kueleweka. Suala hili, lilileta utata na hisia ambazo zimeuletea Ubalozi usumbufu ambao haukuwa na ulazima wowote.

Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania washington DC, inapenda kuwashukuru Watanzania wote waliopo Ndani na Nje ya Nchi waliosaidia katika jitihada za kupatikana kwa taarifa sahihi za mtu huyu. vile vile Ubalozi unazishukuru taasisi zote za hapa Marekani ambazo kwa namna moja au nyingine zimetoa ushirikiano wenye tija uluotuwezesha kulitatua suala hili.

Shukurani za pekee, ziwaendee blogs za vijimambo na swahili villa, bila kuwasahau uongozi wa jumuia ya Watanzania waishio Dallas Texas, Bw Franklin Maji, Mchungaji Absalom na Bi aysha Burnett.
                  IMETOLEWA NA OFISI YA UBALOZI WA TANZANIA
WASHINGTON DC.

Post a Comment

أحدث أقدم