Waliombaka binti Delhi, akapoteza maisha kwa majeraha, wahukumiwa kifo!

 
Wanaume wanne kati ya watano waliotiwa mbaroni kwa makosa ya kupiga, kujeruhi, kubaka na kusababisha kifo cha binti wa miaka 23 mwanachuo katika mji mkuu wa India, Delhi, wamehukumiwa kifo.

Wanaume hao, Mukesh Singh, Vinay Sharma, Akshay Thakur na Pawan Gupta walikutwa na hatia siku ya Jumanne kutokana na makosa waliyoshitakiwa kwayo mahakamani na leo hii Ijumaa wamesomewa hukumu hiyo.

Mmoja kati yao alihukumiwa kutumikia miaka kadhaa kifungoni wiki jana, kutokana na kulindwa na vifungu
vya sheria kwa makosa yanayotendwa na wenye umri wa chini ya miaka 18.

Jaji aliyesoma hukumu hiyo, Yogesh Khanna amesema kesi hiyo iliangukia katika kipengele kisicho cha kawaida na hivyo anatoa hukumu ya kifo, huku akipinga maombi yote ya kufanya wepesi wa hukumu hiyo, mathalani kwa kutoa kifungo cha maisha gerezani. Jaji huyo aliongeza kwa kusema kuwa kitendo kilichofanywa na vijana hao kilitingisha nchi nzima ya India.

Mmoja wa vijana waliohukumiwa alidondosha machozi baada ya kusikia kauli ya Jaji Khanna.

Baba wa marehemu amenukuliwa kusema kuwa amefarijika kwa hukumu hiyo anayosema imetenda haki kwa kifo cha binti yake. Binti huyo alipoteza uhai wiki mbili baada ya jitihada za kumwokoa kutokana na majeraha aliyosababishiwa na vijana hao, kushindikana.

Watu waliokuwa nje ya chumba cha mahakama na maeneo ya karibu wakifuatilia hukumu hiyo walishangilia na kupongeza hukumu hiyo punde tu iliposomwa.

Jopo la mawakili waliowasilisha kesi hiyo mahakamani walishangilia na kujipongeza kuwa wamefanya kazi yao na kupata matokeo stahiki.

Kama ilivyo kwa hukumu zote za vifo, ni sharti Mahakama Kuu ya India ithibitishe kwanza ndipo itekelezwe. Watuhumiwa pia wanayo nafasi ya kukata rufaa katika Mahakama hiyo Kuu na kuomba msamaha wa Rais.

Post a Comment

أحدث أقدم