Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujenzi wa Jengo la Yanga, Francis Kifukwe amesema kituo
cha mabasi yaendayo kasi (DARTS) kilichojengwa eneo Jangwani kipo ndani
ya eneo lao.
Kifukwe aliyasema hayo wakati ya ziara ya Kamati ya Mipango Miji na
Mazingira ya Manispaa ya Ilala jana ilifanya ziara ya ukaguzi Jangwani
kuangalia eneo linaloombwa na klabu ya Yanga kwa ajili ya ujenzi wa
uwanja wake wa kisasa.
Kifukwe alionyesha eneo wanalohitaji kuongezewa mbele ya Kamati ya
Mazingira kuwa eneo lao linafika hadi kwenye kituo cha mabasi ya mwendo
kasi akidai kuwa waongezewe mpaka kwenye bonde la Mto Msimbazi ambako
pia akidai kuna mabomba mawili ya majitaka yanayopeleka maji baharini
moja likiwa la Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL).
“Kile kituo cha mabasi tumeambiwa kipo pale kwa muda, kwa upande huu
tutafika mpaka sehemu ya matairi (karibu na bonde Msimbazi), na upande
huu wa Barabara ya Morogoro, mwisho wa mpaka wetu ni hapa kwenye misufi,
lakini tunaomba mtuongezee mpaka kule barabarani kabisa.
“Mtuzidishie barabarani kwa vile upande huu wa mbele tayari kuna
barabara ya kiwango cha lami imejengwa ambayo inaenda mpaka Kigogo na
inatumika na watu wengi hivyo hii barabara hatutaigusa, na upande huu wa
Barabara ya Morogoro kuna bomba jingine ambalo litaingia ndani ya
uwanja wetu.”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki, Sultan Salum akizungumza mara baada
ya ziara hiyo alisema wamepokea maombi ya Yanga na wameona eneo
wanalohitaji, hivyo watakaa kikao Jumanne ijayo kujadili suala hilo na
kujiridhisha iwapo itafaa kwa Yanga kupatiwa eneo hilo.
“Hili suala lina mlolongo mrefu, kwa sababu sio NEMC tu itabidi
liende mpaka kwa watu wa Ardhi, na Serikali Kuu, sio la kumalizika leo
hili, sisi Jumanne tutakaa wajumbe watakavyoamua tutawapa
majibu.”alisema.
Hata hivyo; tayari ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Ilala
imeshaweka wazi msimamo wake wa kuwataka viongozi wa Yanga kubeba
dhamana ya fidia za watakaoathirika na ujenzi wa uwanja huo na kwamba
gharama halisi itajulikana itakapofanyika tathmini halisi.
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment