Maisha ya ‘Geto’ Changamoto kwa Wanafunzi Sekondari za Kata Tanga

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang'anyo wilaya ya Handeni  wakitembea barabarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji mbalimbali vinavyoizunguka shule hiyo
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang’anyo wilaya ya Handeni  wakitembea barabarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji mbalimbali vinavyoizunguka shule hiyo.
UJENZI wa Sekondari za Kata katika mikoa mbalimbali umesogeza huduma za elimu kwa baadhi ya maeneo. Ipo mikoa ambayo awali ilikuwa na shule chache za sekondari hali ambayo ilifanya wanafunzi wachache kupata fursa ya kujiunga na sekondari. Kwa sasa hali si hivyo tena, mikoa mingi imeongeza idadi ya shule hizo licha ya changamoto kibao inazozikabili shule hizi.
Zipo baadhi ya shule za sekondari zimejengwa mbali kidogo na makazi ya wahitaji kitendo ambacho huwalazimu wanafunzi kutembea muda mrefu asubuhi wakielekea shuleni na baadaye jioni wakirejea nyumbani, hali ambayo ni changamoto kwa wengi wao.
Hata hivyo baadhi ya maeneo shule hizo zimejengwa mbali zaidi na makazi ya watu kutokana na kile kuhudumia vijiji ama vitatu hadi vinne, na hazina mabweni jambo ambalo wanafunzi wanashindwa kuvumilia umbali uliopo kutoka kijiji kimoja hadi kingine hivyo kutafuta mbinu mbadala ya kusogea jirani na shule wanazokuwa wamepangiwa.
Wanafunzi wanaamua kutafuta vyumba vilivyopo jirani na maeneo ya shule walizopangiwa na hivyo kupanga (kukodi chumba). Wenyewe vyumba hivi huviita mageto. Vyumba hivi huwa vidogo na vingine mithili ya vibanda, ambapo bei huwa ya chini zaidi kwa mwezi. Wanafunzi wengine huamua kujikusanya wawili ama zaidi na kuishi pamoja kwenye geto ili kupunguza gharama.
Mageto mbili
Mageto mbili.
Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto baadhi ya maeneo aina hii ya maisha ya wanafunzi ni kitu cha kawaida. Wanafunzi wameamua kupanga kwenye mageto (vyumba mitaani) na kuishi kwa makundi huku wakikabiliwa na changamoto lukuki zinazohatarisha safari yao ya elimu ya sekondari.
Mbwambo Conrad ni Mkazi wa Kata ya Bungu wilayani Lushoto, eneo ambalo lina idadi kubwa ya wanafunzi waliopanga kutoka vijiji vya mbali huku wakihudhuria masomo yao ya sekondari. Anasema eneo hilo kuna wanafunzi wengi ambao wametoka vijiji vya mbali na wamepanga jirsni na shule kwenye kata hiyo kuhudhuria masomo.
Anasema wanafunzi hao wamepangiwa na wazazi wao ili waweze kuhudhuria masomo yao kuepuka umbali wanaotoka kwenye vijiji vyao. “Wanafunzi hawa wamepanga katika baadi ya vyumba na wanaishi kwa tabu sana…wengi wanaingia katika majaribu kutokana na aina ya maisha wanayoishi,” anasema Mzee Conrad.
Anasema wavulana wengi huishia kuwa wahuni maana uangalizi wa wazazi hawana, mara nyingi utawakuta wamekaa vikundi kwa vikundi nyakati za jioni hadi usiku unaweza kufikiri sio wanafunzi. Wanachelewa kulala muda mwingi wanazunguka kwenye majumba ya sinema (vibanda vinavyo onesha picha za video) hivyo wanaishi kwa kujitawala utazani si wanafunzi.
Willson N’gwamizi ni Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muungui wilayani Lushoto, anasema licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali katika shule hiyo suala la wanafunzi kuishi kwenye mageto ni changamoto kubwa kwa shule kwani linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma. Anasema wanafunzi hulazimika kuishi katika vyumba hivyo vya kupanga kutokana na shule nyingi za kata zilizojengwa kutokuwa na mabweni huku zikichukua wanafunzi kutoka vijiji vya mbali.
“…Kifupi suala la wanafunzi kuishi katika mageto linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma…wanafunzi hawa wanapoishi huko hukosa usimamizi wa wazazi na wengine hata hela ya kumudu maisha hayo huwa ni tatizo maana wanatoka vijiji vya mbali na uwezo wa familia zao wakati mwingine hushindwa kuwatimizia mahitaji yote,” anasema N’gwamizi.
Anasema kutokana na uhuru huo wa kukaa kwenye mageto wanafunzi wengine hutoroka na kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya chai na sehemu nyingine wasichana nao huwa huru zaidi kitendo ambacho hushindwa kukabiliana na changamoto za vishawishi mitaani.
Mageto moja
Mageto moja.
“Ukizunguka katika baadhi ya kata unaweza kukuta wanafunzi wa kidato cha pili wamepanga kwenye chumba kimoja, ndani ya chumba hicho wapo wawili hadi watatu…wengine wanatoka katika familia duni hawapewi mahitaji ya kutosha, wengine hujikuta wanashawishika na kuingia mitaani na kujikuta wanakatizwa masomo kwa kutiwa ujauzito,” anasema.
“Kwa kweli mageto ni tatizo, wapo baadhi ya walimu hujitahidi kuwafuatilia huko wanakoishi ili kuhakikisha wanajenga nidhamu ya kiuanafunzi, hata hivyo zoezi hili bado ni changamoto maana na walimu wamejikuta wakikaa mbali na shule kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu jambo ambalo ni tatizo pia…,” anasema mwalimu huyo.
Suala la ukosefu wa mabweni kwa shule za kata na kuwalazimu wanafunzi kupanga mitaani (mageto) halipo kwa wilaya ya Lushoto pekee. Wilaya ya Handeni nayo inakabiliwa na changamoto hiyo ya wanafunzi kupanga uswahilini wenyewe karibu na shule walizopangiwa.
Ester Frank ni mmoja wa wanafunzi wa sekondari za kata wilayani Handeni anasema changamoto kwa wanafunzi kukaa kwenye mageto ni kubwa hasa wa kike. Anasema wengi wanakosa uangalizi na usimamizi hivyo kujikuta wanajiingiza kwenye vishawishi hivyo kuishia kupata mimba na kukatizwa masomo yao. “…Usema kweli mageto yanatuathiri wanafunzi hapa wilayani Lushoto,” anasema mwanafunzi huyo.
Afidha Said ni mkazi wa Kijiji cha Kidereko, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga. Said anasema katika mahojiano na mwandishi wa makala haya kijijini Kidereko wilayani Handeni, aliyekuwa akifuatilia vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo hufanyiwa baadhi ya wanafunzi na wanawake eneo hilo kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa). Anasema matukio ya mimba kwa wanafunzi eneo hilo si kwamba hulazimishwa kimahusiano, bali huingia wenyewe katika mahusiano kingono kutokana na mazingira halisi.
Anasema ukiachilia mbali uduni wa kipato kwa familia nyingi eneo hilo, ambao wengi ndio wazazi/walezi wa wanafunzi, shule nyingi za kata Wilaya ya Handeni zipo mbali na makazi ya wanafunzi. Zimejengwa hivyo ili kuweza kuhudumia vijiji vingi, ambavyo pia kuna umbali mkubwa kutoka kijiji kimoja hadi kingine.
Wapo wanafunzi ambao hulazimika kutembea kilometa 12 hadi 20 kwenda na kurudi shuleni kila siku jambo ambalo linawaumiza wengi, hivyo kulazimika ama kutafuta urahisi wa kupata usafiri hasa kwa wanafunzi wanaotoka vijiji vya mbali au kulazimika kupanga katika mageto jirani na shule walizopangiwa. kwa usafiri maarufu ambao hutumika na jamii maeneo mengi ya vijiji hivi ni pikipiki (bodaboda), ambao wazazi hawawezi kuumudu kwa wanafunzi wao kutokana na gharama za juu.
SAM_2126
Mmoja wa walimu katika moja ya shule za kata wilaya ya Handeni (jina tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji) anasema shule yao inawanafunzi wanatoka katika vijiji kama Kidereko ambacho ni takribani kilomita 6 kwenda na Kijiji cha Bangu ambacho ni karibu kilomita 10 kwenda tu. Anasema umbali kama huu ukiuunganisha mwanafunzi analazimika kwenda na kurudi kila siku unakuta ni tatizo.
Anasema na wengi wanatoka katika familia duni unakuta hawapewi chochote wanapotoka nyumbani kama matumizi ya siku (kula), sasa katika hali kama hii inakuwa tabu. Wapo ambao wanaamua kukata tamaa ya kuendelea na shule hivyo kujiingiza katika mambo ambayo yanawaharibu kitabia kabisa.
Rais Jakaya Kikwete akihutubia wananchi Januari 7, 2013 mjini Igunga aliwahi kusema kuwa serikali inajitahidi kukabiliana na changamoto za elimu. “Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu (2013) tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu ni 57,755 kati yao  20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari. 
Rais Kikwete anasema kwa mwaka 2014 Serikali itaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi. Kwa upande wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi.
Rais Kikwete anasema upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vya ualimu nchini ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka. Anaongeza kuwa mapema mwaka 2014 Serikali itakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hilo.
Hata hivyo licha ya juhudi hizi kwa upande wa changamoto ya walimu hasa kwa shule za kata kuna haja ya Serikali kuangali namna ya kulipa kipaumbele suala la kupambana na changamoto za umbali wa shule za kata na makazi ya wananchi na kuhakikisha ujenzi wa mabweni ili kupunguza adha wanazopata wanafunzi wa kike na kiume kutokana na changamoto hiyo inamalizima kama si kupungua kwa kiasi fulani. Tukiamua tunaweza kukabiliana na changamoto hizi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA

Post a Comment

أحدث أقدم