TCRA yapongeza Ushirikiano wa Vodacom na UmojaSwitch

004 TCRA
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,(TCRA) imesema inafurahishwa na ukuaji na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya simu za mkononi katika
kuboresha maisha ya watu na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Mkuu wa Masoko wa M-pesa Isaac Nchunda (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi huduma mpya ya utoaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya M-pesa kupitia ATM za Umoja inavyofanyakazi muda mfupi baada yauzinduzi rasmi wa huduma hiyo. Wanaoonekana pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof. John Nkoma (wa pili kushoto), Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twissa(wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch Danstan Mbilinyi
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Prof. John Nkoma wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ushrikiano kati ya Kampuni ya Umoja Switch na Vodacom Tanzania kupitia huduma yake ya M-pesa utakao wawezesha wateja wa Mpesa kutoa fedha kupitia ATM za mtandao wa Umoja nchi nzima.
M-pesa ndio huduma inayoongoza miongoni mwa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi ikiwa na mtandao mpana zaidi wa mawakala zaidi ya 65,000 walioenea nchi nzima na hivyo kuiwezesha huduma hiyo kuwa rahisi zaidi kupatikana.
Prof. John Nkoma amepongeza ushirikiano huo katika kile alichokiita kuwa kitaendeleza mafanikio ya ukuaji wa tekonolojia ya simu za mkononi ikiwemo M-pesa huku akitanabaisha kuwa mamlaka yake imekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinarahisisha maisha ya Watanzania kwa kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku iwe katika kilimo na ufugaji, biashara na hata katika masuala ya kifamilia.
“Sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano tumefurahishwa sana kwa ushirikiano huu, katika utoaji wa Leseni tunazo za aina nne moja ya miundombinu, huduma, matumizi na utangazaji. Katika Leseni ya Miundombinu huu ni mfano vizuri wa kutumia teknolojia ambapo sekta ya fedha zinaungana na sekta ya Mawasiliano katika kutoa huduma kwa Watanzania,” alisema Prof. Nkoma na kuongeza.
“Uwepo wa huduma hii utawawezesha Watanzania wengi kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, haya ni maendeleo mazuri sana katika sekta ya Mawasiliano na sekta ya fedha, sasa hizi wananchi wanaweza kuchukua huduma nyingi sana, hili sio jambo dogo hivyo kwa namna ya upekee kabisa ningependa kuwapongeza Vodacom na Umoja Switch kwa kuwezesha Ushirikiano huu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, alibainisha kwamba wateja sasa wanaweza wakatumia mashine za ATM za Umoja Switch sehemu yoyote ya nchi kufanya miamala yao ya kifedha.
“M Pesa imepiga hatua nyingine ya juu zaidi. Wateja wetu sasa hawana wasi wasi tena kwani wanaweza kutoa fedha kutoka katika Akaunti zao za M pesa kupitia ATM za UmojaSwitch mahali popote. Hii ni hatua kubwa tumepiga kwetu sisi wote na tutaendelea kuwaletea huduma na bidhaa nyingi zaidi sokoni,” alisema Twissa na kuongezea kwamba, “M Pesa inaendelea kubadilika kulingana na maendeleo ya kiteknolojia ambayo yamelenga kuihudumia wateja wetu vizuri zaidi.”
Mtandao wa Umojaswitch umeanzishwa mwaka 2006 ukiunganisha benki zaidi ya 24 nchini na ATM takribani 200.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UmojaSwitch Bw.Danford Mbilinyi amesema kuwa anashukuru sana ushirikiano huu na Vodacom na kubainisha kwamba hii itasaidia katika kuwahudumia wateja ipasavyo mahali popote walipo. “Hii ni siku kubwa sio tu kwetu sisi bali hata kwa wateja wetu pia. Ushirikiano huu ni wa aina yake kwetu sisi, na tunawashukuru sana Vodacom kwa kuamua kuja kwetu
sisi,”alisema Mbilinyi.
Mpaka sasa huduma ya M Pesa inayotolewa na Vodacom inajivunia kuwa na mawakala takribani 65,000 waliosambaa nchi nzima, ambao siku zote wapo tayari kuwahudumia wateja wetu. Huduma hii pia imekuwa ikiingia katika ushirikiano na mabenki na makampuni mengine
nchini, wateja wetu sasa wana uwezo wa kununua bidhaa na huduma mbali mbali na kufanya malipo kupitia M-Pesa

Post a Comment

أحدث أقدم