Uamsho yalia na Lukuvi

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Uamsho, Khamisi Yussuf Khamis (Kushoto)akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya kauli ya Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge) William Lukuvi dhidi yao. Katikati ni mjumbe mwingine wa kamati ya Utendaji, Said Amour Salim. Picha: IPP Media
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Uamsho, Khamisi Yussuf Khamis (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya kauli ya Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge) William Lukuvi dhidi yao. Katikati ni mjumbe mwingine wa kamati ya Utendaji, Said Amour Salim.
Picha: IPP Media
Dar es Salaam. Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), imemtumia barua Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kueleza masikitiko yake kuhusu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuwa inahusika na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Lukuvi ambaye ni mjumbe wa Bunge la Katiba alitoa madai hayo bungeni wakati akifafanua kauli alizotoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma kuwa Tanzania ikiingia katika mfumo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi kwa kuwa Serikali ya Muungano itakosa fedha za kuwalipa mishahara.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati Utendaji ya Jumiki, Yusuph Khamis alisema baadhi ya mambo ambayo Lukuvi aliituhumu jumuiya hiyo ni pamoja na mauaji ya padri, kuchomwa kwa makanisa na uharibifu wa mali za umma Zanzibar, mambo ambayo alisema si kweli na ameshindwa kutoa ushahidi kuthibitisha madai yake.
Lukuvi ambaye hivi karibuni alielezwa anakwenda nje ya nchi kwa matibabu, hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo.
Alisema kauli za Lukuvi zinaligawa Taifa kwa misingi ya kidini jambo ambalo lilipigwa vita na waasisi wa Taifa.
Alisema tuhuma kwamba Uamsho inaeneza itikadi za CUF si za kweli kwa sababu jumuiya yao haina ushirika na chama chochote cha siasa, bali inafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Alisema anashangaa kuona Serikali haijatoa tamko lolote juu ya matamshi hayo hali inayowafanya waamini kuwa Lukuvi alitumwa kueneza siasa za kidini ambazo hujenga chuki miongoni mwa wananchi wenye imani tofauti.
Sheikh Khamis alisema mwaka 2004, Jumuiya ya Uamsho ilituhumiwa kuhusika na vurugu zilizotokea Zanzibar ikiwamo milipuko ya mabomu, kuchomwa kwa makanisa, kuchomwa kwa gari la polisi na uharibifu wa miundombinu.
Alisema baada ya matukio hayo, tume mbili; ya Maziwa Makuu na ya Kamati Maalumu ya Jeshi la Polisi ziliundwa kufanya uchunguzi, lakini miaka 10 sasa hazijatoa matokeo ya uchunguzi wao, hali inayowafanya waamini kuwa viongozi wao waliokuwa wakishikiliwa na polisi hawakuwa na hatia.
Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم