Daladala
1,800 zinazofanya safari zake kati ya Kimara na Kivukoni, zinatarajiwa
kuondolewa katika barabara hiyo yenye wateja wengi, baada ya kuanza kwa awamu
ya kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart).
Daladala
hizo zitapangiwa njia nyingine za pembezoni, ambako hakuna wateja, kama
barabara ya awali, huku madereva wake watakaojitokeza kuomba ajira,
watapewa kipaumbele katika mabasi ya kasi.
Meneja
Uendeshaji wa Dart, Peter Munuo, alisema hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari, kuhusu maendeleo ya mradi huo.
"Daladala
hizo zitapangiwa ruti mpya, kama mnavyojua hapa kwetu (Dar es Salaam) usafiri
ni wa tabu kidogo, hasa kwa maeneo ambayo yako pembezoni," alisema Munuo.
Meneja
Msimamizi wa Matumizi ya Barabara wa Dart, Mohamed Kuganda, alisema mradi huo
unatarajiwa kukamilika mwaka kesho.
Lakini,
alisema jambo hilo litawezekana, endapo mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo,
Kampuni ya Strabag, atakomesha migogoro inayoendelea.
Alisema
kwa sasa kampuni hiyo, imekuwa ikiingia katika migogoro na wafanyakazi wake,
jambo ambalo kama kampuni hiyo haitachukua hatua za haraka, linaweza kukwamisha
mradi huo kukamilika kwa wakati.
"Tunataka
wakae na wafanyakazi wao, wajadili kwa sababu migogoro hii, inaathiri maendeleo
ya mradi wakati mitambo ipo, lakini haifanyi kazi na hivyo inaweza kuchelewesha
kazi," alisema Kuganda.
Alisema
mradi huo, unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo maandalizi ya
huduma za awali.
Alisema
kuwa wanatarajia kuanza kutoa huduma za awali kwa mabasi makubwa 20 na madogo
10. Alisema zinahitajika Sh bilioni 20 ili kufanikisha hatua za awali za kuanza
mradi huo.
Meneja
Uhusiano wa Dart, William Gatamba, alisema madereva daladala, watakaopewa
vipaumbele watapelekwa katika mafunzo maalumu, ambapo baada ya hapo vigezo
ndiyo vitawawezesha kupata ajira.
Post a Comment