Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste
Zanzibar, wamemsifu Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala kuwa ni kiongozi
anayejali Muungano na kumtabiria makubwa katika safari yake ya kisiasa nchini.
Viongozi hao wa dini, walisema hayo
juzi wakati wa Tamasha la Amani na uzinduzi wa albamu ya Jiwe ni Jiwe ya
Kwaya ya Tumaini ya Kanisa la Pentekoste Tanzania (FPCT).
Tamasha hilo lilifanyika kwenye
Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, ambako Dk Kigwangala alikuwa mgeni
rasmi.
Askofu wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG), Dk Dickson Kaganga, akimkaribisha Mbunge Kigwangala
alisema kitendo cha Mbunge huyo kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika
tamasha hilo Zanzibar, kinaonesha jinsi alivyo muumini wa Muungano.
“Umetoka mbali sana kule Nzega,
umevuka maji hadi huku Zanzibar, umeonesha upendo sana na kwa sababu kuna
amani, tunashukuru Mungu kwa kukufikisha salama.
Kwa kitendo hiki cha upendo,
tunakutabiria makubwa siku za usoni na tunakuombea kwa Mungu akufanikishie,”
alisema Askofu Kaganga, maarufu Mzee wa Viwango na Uwiano.
Akizungumza katika tamasha hilo,
Kigwangala aliwataka waumini wa madhehebu mbalimbali nchini, kuendeleza amani
iliyopo kwa kuwa imetokana na uimara wa Muungano wa nchi mbili, ambao umedumu
kwa nusu karne sasa.
Alisema wako watu, hawapendi kuwepo
kwa Muungano na kuwataka Watanzania wasiwape nafasi ya kuuvunja.
Dk Kigwangala alisema siku zote,
waumini wa dini mbalimbali wanapenda amani na kuonya kuwa kama amani ikitoweka,
italeta mfarakano.
Alisema ametoka Tanzania Bara kwenda
kuzindua Tamasha hilo Zanzibar, kutokana kuwepo kwa Muungano, ulioasisiwa na
Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Shekhe Abeid Amaan Karume wa
Zanzibar.
Katika tamasha hilo, Mbunge huyo
alinunua albamu tatu kwa Sh 1,000,000 kuunga mkono mafanikio ya Kwaya ya Tumaini
ya kanisa hilo.
Post a Comment