Serikali inatarajiwa kuajiri
mahakimu wapya zaidi ya 300 katika mwaka ujao wa fedha 2014/ 2015 na mwaka
unaofuata wa 2015 /2016, itaajiri mahakimu wengine 300.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo
jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Chama cha
Majaji Wanawake Duniani.
Mbali na ajira hizo, Rais Kikwete
pia alisema hivi karibuni anatarajia kuteua tena majaji 20 wa Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufaa, pamoja na kujenga Mahakama Kuu katika mikoa minne ili
kuendelea kuboresha Mahakama.
Alisema Serikali imejitahidi
kuongeza rasilimaliwatu katika Mahakama, ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2005
kulikuwa na majaji 45, kati yao wanawake walikuwa 10, wakati sasa kuna majaji
78 na kati yao wanawake 30.
Hata hivyo, Rais Kikwete alieleza
kwamba maboresho katika Mahakama, hayawezi kufanikiwa, bila kushirikisha
sekta nzima ya sheria.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete
aliwatahadharisha watoa haki mahakamani, kuacha kuegemea kuwapa au kutoa haki
kwa watu wenye uwezo kiuchumi, hata kama haki hiyo, si yao.
Alisema si busara kwa mhimili wa
Mahakama, kutoa haki kwa watu wenye uwezo hususani kiuchumi huku wanyonge
wakikosa haki hiyo.
Pia, aliutaka mkutano huo, utumike
kusaidia kuboresha shughuli za Mahakama ili zitoe haki sawa na kurekebisha
sheria mbalimbali, zilizoridhiwa kutoka kwa Wakoloni ili sheria za Tanzania
ziendane na mazingira ya nchi.
Rais wa Chama cha Majaji Wanawake
Duniani (IAWJ), Jaji mstaafu Eusebia Munuo, alisema mkutano huo, utatoa
fursa kwa majaji kubadilishana uzoefu, utakaosaidia katika utendaji wao wa kazi
za kimahakama.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete alikwenda Kituo cha Uhamilishaji wa Mbegu
Bora za Madume ya Ng’ombe kilichopo Usa River, kujionea maendeleo ya
kituo hicho na kuangalia ng’ombe aliyemtoa wiki moja iliyopita kwa kituo hicho
kusaidia kutoa mbegu bora .
Post a Comment