Uamuzi wa ombi la Mbunge wa Bahi,
Omary Badwell (CCM), kwamba usikilizwaji wa kesi inayomkabili ya kuomba
na kupokea rushwa ya Sh milioni nane usitishwe, utatolewa Mei 12 mwaka
huu.
Uamuzi huo ulipaswa kutolewa jana na
Hakimu Mkazi Hellen Riwa, lakini iliahirishwa kwa sababu Hakimu huyo ana
udhuru.
Badwell aliomba kesi hiyo isiendelee
kusikilizwa, kwa kuwa amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, kuhoji kifungu cha sheria kinachokataza mshitakiwa katika kesi za jinai
kukata rufani.
Kupitia kwa Wakili wake Mpare Mpoki,
Badwell alidai wamefungua kesi hiyo kwa kuwa kifungu hicho kinapingana na Ibara
ya 13(6)(a) ya Katiba, ambayo inampa haki mtu yeyote kupinga uamuzi wowote
ambao anaona utamuathiri.
Aidha anaiomba Mahakama Kuu itamke
kifungu hicho ni batili na kinapingana na Katiba kwa kuwa Mahakama ya Kisutu
haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya kikatiba.
Wakili Mpoki alidai wakiendelea
kusikiliza kesi hiyo, wataendelea kuvunja haki ya mshitakiwa, ambayo tayari
ilishavunjwa na kuomba kesi hiyo isimamishwe hadi watakapopata uamuzi wa
Mahakama Kuu.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa kati
ya Mei 30 na Juni 2 mwaka 2012, katika maeneo tofauti Dar es Salaam, mshitakiwa
alishawishi apewe rushwa ya Sh milioni nane kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
Ilidaiwa kwamba Badwel aliomba
rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani
Pwani. Pia anadaiwa Juni 2, 2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Ilala,
alipokea rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa Sipora.
إرسال تعليق