Mashahidi wa upande wa mashitaka
katika kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4,
inayowakabili raia watatu wa China, wataendelea kutoa ushahidi Mei 13 na 14
mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washitakiwa hao ni Huang Gin (50),
Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), wote wakazi wa eneo la Mikocheni B,
Barabara ya Kifaru, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi
alidai jana mbele ya Hakimu Mfawidhi Isaya Arufani, kuwa kesi hiyo
imekuja kwa kutajwa na kuomba tarehe nyingine ya kuendelea kusikilizwa.
Hakimu Arufani aliahirisha kesi hiyo
hadi Mei 13 na 14 mwaka huu, watakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa
mashitaka.
Hivi karibuni mahakama hiyo, ilitoa
amri kwa waandishi wa habari, kutoandika mashahidi wa upande wa mashitaka kwa
ajili ya usalama wao.
Alidai kuwa Novemba 2, mwaka jana katika
mtaa wa Kifaru Mikocheni B, washitakiwa walikamatwa wakiwa na vipande 706 vya
meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,889 vyote vikiwa na thamani hiyo, mali ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi
wa Wanyamapori.
Alidai katika mashitaka mengine,
wanadaiwa kutaka kutoa rushwa ya Sh milioni 30.2 kwa askari Polisi na askari wa
Wanyamapori ili wasifunguliwe mashitaka.
Katika mashitaka mengine,
washitakiwa wanadaiwa siku hiyo hiyo walikutwa na ganda la risasi bila kuwa na
kibali cha kumiliki silaha. Washitakiwa hao walikana mashitaka yao na
kurudishwa rumande hadi Februari 17 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
إرسال تعليق