Balozi Seif Afanya ziara Jimboni kwake na kukabidhi Vifaa mbalimbali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taasisi na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya mafuta na gesi yameanza kujitokeza kuomba fursa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutaka kuwekeza katika sekta ya mafuta na Gesi.

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Al Iddi akikagua mradi wa maji safi na salama wa Kijiji cha Kichungwani Jimbo la Kitope mara baada ya kushiriki kazi za ujenzi wa Taifa za kulaza Bomba la Maji.
Alisema maombi ya mashirika na Taasisi hizo yamekuja kufuatia suala la mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Muungano kwenye katiba iliyopendekezwa na bunge maalum la Katiba lililomaliza kazi zakehivi karibuni Mkoani Dodoma.

Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alitoa kauli hiyo mara baada ya kushiriki katika kazi za ujenzi wa Taifa za kulaza Bomba la Maji safi katika Kijiji cha Kichungwani lililoanzia katika Kijiji cha Kitope.

Kazi hiyo ilikwenda sambamba na Balozi Seif kukabidhi Vipando vya usafiri aina ya Vespa kwa ajili ya kuwarahisishia kazi Viongozi wa wadi Nne zilizomo katika Jimbo la Kitope pamoja na kukabidhi msaada kwa familia Tatu zilizokumbwa na maafa ya upepo pamoja na moto ukapelekea nyumba zao kuathirika.

Vifaa pamoja na mchango huo wa Balozi Seif uliojumuisha pia fedha za ununuzi wa madirisha ya Tawi la CCM Kichungwani na Timu ya Soka ya Kijiji hicho umegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 16,850,000/-.

Balozi Seif alisema wananchi hao pamoja na Wazanzibari wote wana fursa za kuunga mkono juhudi zilizochukuliwa na Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba za kuiunga mkono Katiba iliyopendekezwa kwa kuipigia kura ya ndio itapowasilishwa kwao wakati wa kura ya maoni.


“ Nawaomba Wananchi na wapenda amani wote nchini kuiridhia Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ili imalize kiu iliyokuwepo kwa muda mrefu “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Katiba hiyo itatoa nafasi na fursa pana kwa Zanzibar katika kuimarisha mfumo wake wa kiuchumi na ustawi wa jamii mambo ambayo yatawezesha kuondoa kabisa kero za muungano.

Alieleza kwamba Zanzibar endapo katiba hiyo itakubalika kwa umma itaweza kufanya mashirikiano ya moja kwa moja na Taasisi, jumuiya na hata mataifa mbali katika kujiletea maendeleo yake.

Alisema mfumo huo utampa haki Waziri au Kiongozi ye yote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda popote Duniani kutafuta mkopo au misaada bila ya kuingiliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Seif liwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Kichungwani kwa jithada zao za kujiletea maendeleo yao pamoja na kuondosha kero zinazowakabili likiwemo suala la maji safi na salama.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba uongozi wa Jimbo hilo utakuwa tayari wakati wote kuunga mkono jitihada za wananchi hao pamoja na kujaribu kusaidia kuwatafutia wahisani wa kusaidia miradi yao.

Alisema juhudi za awali zimeshaanza kuchukuliwa na uongozi wa jimbo hilo katika kutatua kero ya bara bara na huduma za umeme kwa kuziomba taasisi zinazohusika na miradi hiyo kuchukuwa jitihada za kutatua kero hizo huku akiwataka wananchi wenyewe wajikubalishe kuchangia miradi hiyo.

Akigusia suala la ardhi ambalo limeingizwa ndani ya Katiba iliyopendekezwa kuwa la Muungano Balozi Seif alisema hatua hiyo imezingatia kutoa fursa kwa Wazanzibari kuweza kumiliki ardhi upande wa Tanzania Bara ili waendelee kuimarisha harakati zao za kiuchumi.

“ Wazanzibari wapata hasara kubwa kama katiba iliyopendekezwa hawataiunga mkono na kuipigia kura wakati utakapowadia “. Alisema Balozi Seif ambae alikuwa Mbunge wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Jimbo la Kitope.

Naye Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwaomba wananchi hao kujikubalisha kuwa walinzi wa miradi yao ili kuwadhibiti watu wanaojaribu kuvuruga miradi yao ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Mama Asha alisema wapo baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wanaojaribu kuwadanganya wananchi wasishiriki katika miradi yao ya maendeleo wakijisahau kwamba wanasiasa hao sio viongozi bali ni watumishi wa wananchi.

Mama Asha aliwaahidi Wananchi hao wa Kijiji cha Kichungwani kwamba atakamilisha kuchangia maroli matano ya Mipira ya maji ili kukamilisha mradi wao wa huduma za maji safi unaotokea katika Kijiji cha Kitope hadi Kijijini pao Kichungwani.

Mapema Sheha wa Sheria ya Kitope Kichungwani Bwana Bakari Khamis Simai alisema kwamba mradi huo wa maji safi na salama hivi sasa tayari umeanza kuwafaidisha wananchi hao kwa zaidi ya robo tatu.

Bwana Bakari alieleza kwamba huduma za maji safi zilizokuwa kero na usumbufu mkubwa wa muda mrefu kwa wakaazi hao wa Kichungwani hivi sasa imekuwa ikipatikana katika pindi choche cha saa ishirini na nne.

Chanzo: zanzinews.com

Post a Comment

أحدث أقدم