CCM tupo Imara ZNZ-Vuai Ali Vuai


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kiko imara kisiasa Zanzibar, hivyo wanachama wake wasiwe na hofu.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, jana alipokuwa akifungua semina ya sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na makatibu wa mikoa na wilaya wa chama hicho.
Alisema mara nyingi wanapoelekea katika chaguzi mbalimbali kunakuwa na hofu kubwa kwamba upande wa Zanzibar itakuwaje.
“Napenda niwaambie kwamba hali ya Zanzibar kisiasa ni shwari na nataka nithibitishe hilo kwa kupitia chaguzi ndogo kule Zanzibar zilizofanyika baada ya uchaguzi mkuu 2010 ambazo zilifanyika nne, tatu tumeshinda kwa kishindo haijawahi tokea tumeshindwa moja,” alisema Vuai.
Vuai alisema CCM itaendelea kushinda kutokana na mipango na si ubabe na kwa haki kwani hali hiyo inatokana na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama ambayo imesimamiwa ipasavyo na watendaji wake.
“Lazima tuhakikishe tunapata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mkuu Tanzania bara na Zanzibar na tupate ushindi wa kishindo kwa haki na si kwa ubabe kwa kuzingatia sheria za uchaguzi na miongozo inayotolewa katika uchaguzi unaohusika,” alisema.
Alisema hawatashinda kwa ubabe kwani wanawakilisha wananchi na wanawafanyia wanayoyatarajia katika utekelezaji wa Ilani hiyo ambao umefanyika vizuri.
Kuhusu Katiba inayopendekezwa, alisema kwa uwezo wa Mungu suala la kuhakikisha theluthi mbili kutoka kila upande inapatikana limewezekana, hivyo hakuna jambo litakaloshindikana.
Katibu wa NEC wa Oganaizesheni, Dk Mohamed Seif Khatib, alisema lengo la semina hiyo ni kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu.
Alisema ni muhimu kushinda uchaguzi huo kwa kuwa itapigwa kura ya maoni kabla ya uchaguzi mkuu.
Pamoja na Khatib kusema kura ya maoni itafanyika kabla ya uchaguzi mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijatangaza muda wa kura hiyo, ingawa makubaliano kati ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa ni kura hiyo kufanyika baada ya uchaguzi mkuu.
“Tumekutana hapa kwa ajili ya vita kubwa ya uchaguzi tunataka kila mmoja atimize wajibu wake kwani mtapimwa utendaji wenu kutokana na ushindi tutakaoupata katika uchaguzi, ambaye atapoteza kata ajue kuwa ndicho kipimo chako na hufai, hivyo mkajipange vizuri,” alisema Dk. Khatib.
(Nipashe)

Post a Comment

أحدث أقدم