China yafadhili wanafunzi 22 shahada ya kwanza

Na Hafsa Golo
Wanafunzi 22 wanaokwenda masomoni nchini China, wanaondoka nchini kesho na Alkhamis tayari kuanza masomo yao ya shahada ya kwanza kwa kipindi cha miaka minne. 
Wanafunzi hao watajifunza kada za habari, mafuta, biashara na fedha.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Juma Shamuhuna, aliwakabidhi wanafunzi hao tiketi za ndege.

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu Zanzibar, Iddi Khamis Haji, alisema wanafunzi hao walipatiwa jumla ya shilingi milioni 25 kwa ajili ya gharama za chakula.

Aidha alisema kati ya  wanafunzi hao wanafunzi 12 watasomea fani ya habari katika njanja ya picha,video, uhandisi wa televisheni pamoja na masomo ya utangazaji.

Wanafunzi hao watasoma Chuo Kikuu cha  ZHEJIANG.
Alisema na wanafunzi wengine  10 watasoma Chuo Kikuu cha ZUNYI katika fani za mafuta,fedha,uongozi,ualimu na biashara.


Aidha alisema masomo hayo yatagharamiwa na  serikali ya China.
 Naye Profesa Li Xiany kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) aliwata wanafunzi hao kufuata taratibu za masomo na kusoma kwa bidii ili lengo lililokusudiwa  la kuongeza wataalamu wa fani mbali mbali liweze kufikiwa.

Alisema suala la heshima na uwajibikaji ndivyo vitakavyoleta ufanisi wa masomo yao.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, aliwata wanafunzi hao kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Kizanzibari ili waweze kuwa wawakilishi wazuri katika kuitangaza nchi yao.


Aliwataka watakapofika China ni vyema kwenda kujisajili katika ubalozi wa Tanzania,kwa ajili ya usalama wao na pia kutatuliwa matatizo yao

Post a Comment

أحدث أقدم