Kweli dunia ina mambo! Kuna watu wanajaribu kutumia kila fursa inayopatikana kujinufaisha kwa kupata fedha hata ziwe ‘chafu’, kwao kitu cha maana ni kupata utajiri kwanza.
Sunday Bekunda
Kundi la watu wanaofanya biashara ya kusafirisha watu, wamekuwa wakitumia fursa ya ukosefu wa ajira kama chambo cha kuwanasa vijana na kuwaingiza kwenye biashara haramu kama ukahaba.
Hivi karibu kundi hilo linalosafirisha watu lilipita katika vyuo vikuu kadhaa nchini Uganda na kuwaahidi wanafunzi kuwa lingewatafutia kazi Ulaya na Marekani, kwani lina uzoefu wa kutosha na kazi hiyo. Mmoja wa vijana ‘waliobahatika’ kupata nafasi ya kwenda Ulaya kufanya kazi ni Sunday Bekunda (25), mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala.
Kwa bahati mbaya ‘neema’ ya kwenda Ulaya iligeuka balaa baada ya kutekwa na kulazimishwa kufanya ngono na wanawake mbalimbali huku akirekodiwa kwenye kamera za video.
“Ilikuwa ni Januari 2013, nilipokutana na mwanaume mmoja anayeitwa Charles kutoka katikati ya Jiji la Kampala, ambaye aliniahidi kunipeleka Kenya kufanya kazi katika kiwanda.
Sikujua kuwa Charles alikuwa msafirisha watu. Alikuwa anaonekana kama mzazi wa makamo aliyefanya kazi kwa miaka mingi.
Nilifungua moyo wangu na kumweleza changamoto nyingi ninazopitia na namna nilivyo hangaika kutafuta kazi ili nipate fedha za kulipia masomo ya ziada. Kwa kifupi ni kama nilikuwa namwambia Charles kuwa sikuwa natafuta kazi bali nilikuwa nataka kazi yoyote.”
Safari ya Kenya
“Siku iliyofuata nilikuwa tayari kwa safari na nilimkuta Charles akiwa kwenye gari la binafsi aina ya Toyota Noah. Alikuwa pamoja na wasichana sita na wavulana wawili. Alituambia kuwa tutaingia Kenya kwa kupitia mpaka usio rasmi unaoitwa Chepskunya.
Tukiwa njiani, Charles alikuwa anaongea sana na kutusisitizia kuwa ‘tusimwangushe’ tukifika huko. “Tulipofika Kenya walituchukua na kutuingiza kwenye nyumba moja nzuri ya makazi ya watu, hapo tulikutana na wenzetu 15, wavulana wawili kutoka Rwanda na Wakenya 13.”
Kutekwa
“Charles alituacha hapo tukiwa chini ya mwanamke mmoja na wanaume wanne wenye miili iliyojengeka vyema. Watu hao walianza kutupiga makofi na kutulazimisha tuvue nguo. Ndipo nilipobaini kuwa kilichoonekana kama ni safari sasa imegeuka utekaji.
Baada ya kupigwa tuliambiwa tutoe mifukoni kila kitu tulichokuwa nacho na kuweka juu ya meza. Nilishtushwa nilipoona vyeti vya wanafunzi wa Uganda kutoka Vyuo Vikuu vya Kyambogo, KIU (Kampala International University), Nkumba na UCU (Uganda Christian University). Hata vyuo vya Kenya vilikuwapo.
Mwanamke alitutishia kutuua kama tusingetii walichosema. Kudhihirisha alichokuwa anamaanisha, alituonyesha mkanda wa video wa mtu akiuawa na kupasuliwa tumbo. Halafu wakaweka video vyingine iliyotuonyesha biashara tutakayokuwa tunaifanya, ambayo ni kuigiza picha za ngono.”
Ratiba ya kufanya ngono
“Walituongoza hadi ghorofa ya juu na kutuweka katika vyumba tofauti. Katika chumba nilichokuwepo aliingia mtu na kuniambia nitoe nguo kisha akanipa chupi tatu zinazobana. Hicho chumba kilikuwa na mwanga mkali na kamera za CCTV katika kila kona. Baadaye wakamleta Bridget, mmoja wa wasichana niliotoka nao Uganda, kisha wakaniambia kuwa nipo huru kufanya naye ngono. Walipoondoka na kufunga mlango, Bridget alianza kulia na kupiga kelele.
Matukio mabaya yalianza rasmi siku iliyofuata wakati yule mwanamke alipoingia kwenye chumba changu akiwa ameshika mikanda mitatu ya ngono. Baadaye waliletwa wanawake na wanaume niliokuja nao nikaambiwa nifanye nao ngono wakati watu wengine wakirekodi kwa kutumia kamera kubwa.
Nilipoishiwa nguvu, yule mwanamke alitoka nje na kurudi halafu alinichoma sindano yenye dawa ambayo ilinifanya nipate nguvu tena na kuendelea. Nikapewa ratiba ya kulala na wanawake asubuhi, wavulana jioni (mashoga) na wanawake watu wenye umri mkubwa usiku.
Wanawake hao walikuwa wanawalipa wale jamaa ili tufanye nao ngono. Kuna wakati nilikuwa nalazimishwa kulala na wanawake saba kwa siku huku nikipata maumivu makali.”
Mauaji
“Baada ya wiki tatu wote tuliitwa sebuleni na kupewa taarifa kuwa mmoja wetu, aliyeitwa Sam Muteesi kutoka Uganda, alikuwa amekataa kuwatii kwa hiyo alitakiwa auawe mbele yetu. Walimfunga kwenye kiti, japokuwa alikuwa akiomba sana msamaha walimfunika usoni kwa kutumia begi hadi alipokufa.
Kwa kipindi chote cha Januari na Februari 2013, nilikuwa nikifanya ngono za kila aina kila siku huku nikitumia dawa za kulevya na pombe.Mwanzoni mwa Machi, Charles alikuja kwenye chumba changu na kuniambia kuwa ninatakiwa kwenda kuoa Uingereza. Halafu akafungua kompyuta yake na kunionyesha picha ya mwanaume mzee mzungu.
Akaniambia nipite mbele ya kompyuta hiyo nikiwa nimevaa chupi nilizopewa ili huyo mzungu anione (kupitia Skype) kama nifaa.
Huyo mzungu alinipenda, hivyo Charles akawa amepata ‘dili’ ambayo ingenipeleka Uingereza, lakini kwa kuwa sikuwa Mkenya nilitakiwa nirudi Uganda kuchukua hati ya kusafiria”.
Atoroka
“Wakati tukivuka mpaka kuingia Uganda, nilifanikiwa kukimbia pale Mbale tulipokuwa tumesimama kunywa chai. Nilitoa taarifa yangu na kufunguliwa faili namba SD REF 65/19/03/2013. Kwa kuwa Charles alikuwa mtu mwenye nguvu (kifedha) hakufanywa chochote.
Kutokana na mateso niliyopitia nilikuwa kama kichaa, nililazwa katika Hospitali ya Vichaa ya Butabika na nilipewa matibabu kati ya Agosti na Desemba 2013. Pia nilipimwa vipimo vingine na kugundulika kuwa nilikuwa na maambukizi yote makubwa ya magonjwa ya zinaa.“Nimeamua kusimulia habari yangu kama sehemu ya kampeni ya kuwaonya vijana wa vyuo vikuu kuwa makini na watu wanaowaahidi kuwatafutia kazi nje ya nchi.”
Imeandaliwa na Goodluck Eliona kwa Msaada wa Redio Netherlands Worldwide (RNW)
Chanzo: Mwananchi
إرسال تعليق