RAIS KIKWETE AONGOZA SHUGHULI YA KUAGA MWILI WA DKT SHIJA VIWANJA VYA KARIMJEE JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima zake za mwisho kwa mwili wa Marehemu Dkt William Shija alipoongoza shughuli za kuaga leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole Mama Getrude Shija, Mjane wa  Marehemu Dkt William Shija alipoongoza shughuli za kuaga leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka sahihi kitabu cha maombolezo cha msiba wa  Marehemu Dkt William Shija alipoongoza shughuli za kuaga leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimwelekeza jambo ofisa wa Bunge wakati wa shughuli za kutoa heshimam za mwisho kwa Marehemu Dkt William Shija alipoongoza shughuli za kuaga leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Bw. Saidi Yakubu, MC wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu Dkt William Shija leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Anne Makinga akiongea wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu Dkt William Shija leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
Sehemu ya waombolezaji
Rais Kikwete akipeana mikono na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) baada ya kutoa salamu za rambirambi kutoka makao makuu ya CPA jijini London. 
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) akimkabidhi binti wa marehemu vitabu vya maombolezo vilivyotiwa saini na waombolezaji huko London Uingereza.
Familia ya marehemu Dkt William Shija wakiwa  katika shughuli za kuaga mwili leo Jumapili Oktoba 12, 2014 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Oktoba 12, 2014, ameungana na waombolezaji  kutoa heshima za mwisho na kuaga mwili wa Katibu Mkuu wa Kwanza Mwafrika wa Chama cha Mabunge ya Jumuia ya Madola (CPA) Dkt. William Ferdinand Shija, ambaye pia alipata kuwa Waziri  Mwandamizi wa Serikali,  katika shughuli iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Rais Kikwete amewasili kwenye Viwanja vya Karimjee kiasi cha saa 4:10 asubuhi kujiunga na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mwenyekiti wa CPA-Kanda ya Afrika Mheshimiwa Anne Makinda ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, viongozi na wananchi kutoa heshima za mwisho.
Baada ya kuaga mwili, Rais Kikwete ametia saini Kitabu cha Maombolezo ya Dkt. Shija ambaye alifariki dunia Jumamosi ya wiki iliyopita, Oktoba 4, 2014 kwenye Hospitali ya Charing Cross mjini London, Uingereza ambako alikuwa anapata matibabu ya ugonjwa wa Saratani. Makazi yake ya kazi yalikuwa huko huko Uingereza.
Miongoni mwa waombolezaji wengi kwenye shughuli hiyo ya leo ulikuwa ni ujumbe mzito wa CPA ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Lindiwe Maseko wa Afrika Kusini. Pia shughuli hiyo imehudhuriwa na Bwana Joe Omoldin ambaye sasa ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Dkt. Shija ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Nyalukomba, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Aprili 28, Mwaka 1947, alipata elimu ya awali maeneo ya kwako kabla ya kujiunga na Sekondari ya Chopra mjini Mwanza kwa elimu ya sekondari na kuhitimu ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Chan’gombe cha Dar es Salaam Mwaka 1968.
Baadaye, Dkt. Shija alipata Shahada ya kwanza ya Uzamili ya Uandishi wa Habari nchini India kabla ya kupata Shahada ya Uzamivu ya fani hiyo hiyo ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Howard cha mjini Washington, D.C., Marekani. Wakati wote wa masomo yake alikuwa Mhadhiri wa Uandishi kwenye Chuo cha Nyegezi, Mwanza.
Dkt. Shija aligombea na kushinda Ubunge wa Jimbo la Sengerema Mwaka 1990 na kuingia Serikali ambako alishikilia nafasi tofauti kwa vipindi tofauti  kama Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Habari na Utangazaji, Waziri wa Nishati na Madini na Waziri wa Biashara na Viwanda.  Dkt. Shija pia amepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Katika Mkutano Mkuu wake wa 52, Desemba, Mwaka 2006 mjini Abuja, Nigeria, Dkt. Shija alichaguliwa, baada ya mchuano mkali sana,  kuwa Katibu Mkuu wa Kwanza Mwafrika wa CPA, taasisi ambayo tokea kuanzishwa kwake Mwaka 1911 ilikuwa haijapata kumchagua Mwafrika kuwa Mtendaji Mkuu wake.
Alichaguliwa kwa kipindi cha pili Mwaka 2012 baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano. Alikuwa anamaliza muda wake Desemba 2016.
Mpaka anaaga dunia, Dkt. Shija alikuwa ameshikilia nafasi ya Ukatibu Mkuu wa CPA kwa mafanikio makubwa sana kwa miezi saba na miezi tisa. Atazikwa kesho, Jumatatu, Oktoba 13, 2014 katika kijiji cha kwao cha Nyalukomba, Sengerema, Mwanza.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
12 Oktoba,2014

Post a Comment

أحدث أقدم