Muziki wa Bongo Fleva unazidi kubadilika kila kukicha, zile zama
za kufanya muziki wa ‘play back’ unaanza kupotea taratibu na sasa
imefika wakati wa kupiga laivu ambapo kwa staa wa muziki wa Bongo Fleva,
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ atalifanya hilo Sikukuu ya Krismasi
mwaka huu ndani ya Dar Live, Mbagala-Zakhem jijini Dar.
Katika mahojiano yake na gazeti hili Diamond
alizungumza mengi kuhusiana na muziki wake ambapo hakusita kueleza
dhamira yake ya kuubadilisha muziki wake na kuwa ‘live’.
Katika makala haya Diamond anafunguka nyuma ya pazia kuhusiana na maisha ya muziki wake wa sasa.
Changamoto
Miongoni mwa changamoto alizowahi kukutana nazo Diamond tangu afanikiwe kufanya muziki na wanamuziki wa kimataifa ni lugha.
Diamond anakiri kuwa Kiingereza ilikuwa changamoto
kubwa sana kwake na amewasihi sana wanamuziki kutoka Bongo hasa
wanaojitanua kimataifa kulifanyia kazi suala la lugha kwani ni muhimu
sana.
Changamoto nyingine ambayo amekumbana nayo ni
kutokana na suala zima la kutengeneza video. Alikuwa akihitaji kampuni
kubwa ya kutengeneza video ya ‘Mdogomdogo’ lakini kila kampuni aliyokuwa
akikutana nayo walikuwa wakimpigia hesabu kubwa huku wengine
wakimwambia inahitaji kutafuta hekalu kubwa, kijiji kizima jambo ambalo
kwake lilikuwa si rahisi.
“Kwa mara ya kwanza nilikutana na Kampuni ya The
God Father nchini Afrika Kusini ambapo tulikuwa wasanii kama 19 katika
kutengeneza video ya Wimbo wa Cocoa na Chocolate ambao ulikuwa
ukihamasisha kilimo kwa vijana na kuwa kilimo kinalipa.
Tukiwa katika kuchukua vipande vya video sikuwa na
wazo kufanya kazi na kampuni hiyo lakini mmoja wa waandaaji wa kampuni
hiyo alinitaka kubaki baada ya kutengeneza wimbo huo. Kweli niliongea
naye na kusema wananikubali kwa jinsi ninavyoweza kujituma katika
utengenezaji wa video ndipo tukaanza rasmi kufahamiana nao kwa
kutengeneza nao video kama ‘Mdogomdogo’ na ‘Nitampata Wapi’ na
nyinginezo.
Usiku wa Historia
Katika usiku unaotambulika kama Usiku wa Wafalme
ambao unatarajiwa kufanyika ndani ya uwanja wa taifa wa Burudani, Dar
Live, Desemba 25, wiki ijayo. Diamond atapanda na kufanya bonge moja la
shoo la kihistoria.
“Nahitaji kuonyesha Watanzania kwamba tunaweza
kufanya shoo kubwa hata kama tukiwa nyumbani kwetu. Mara nyingi shoo
zangu kubwa huwa zinatoka Dar Live na siku hiyo niwahakikishie kwamba
nitapiga live band nyimbo zote na pili nitakuwepo na wasanii wote
nilioshirikiana nao katika nyimbo zangu huku nikipiga nao hizo nyimbo
jukwaani. Mashabiki pia wategemee kuona madansa wangu wapya na niwaambie
pia nitapiga nyimbo zaidi ya 20 bila kupumzika.”
إرسال تعليق