Haki za binadamu ni stahili maalumu anazopaswa kuwa nazo. Serikali inapaswa kuziheshimu na kuzilinda.
Umoja wa Mataifa unafafanua haki za binadamu
kwamba ni dhamana za kisheria kwa watu wote inayowalinda dhidi ya
vitendo na uondoaji unaoingilia uhuru, stahili na utu wa binadamu.
Mifano ya haki za binadamu ni kuishi, kumiliki
mali, kuchagua viongozi, kupata elimu, kupata afya, ulinzi sawa wa
kisheira, haki ya kuchangamana, kuoa au kuolewa, kutoa maoni, kufuata
imani na utamaduni unaotaka, kuchaguliwa kuwa kiongozi, kusikilizwa na
kutambuliwa na nyinginezo.
Ufafanuzi sahihi wa nini maana ya haki za binadamu kwa wananchi wa kawaida ni mdogo sana.
Pia, kutokana na hilo haki katika baadhi ya wananchi inaonekana kama ni hadhi ya viongozi tu.
Wengine wanatambua haki ni kaulimbiu tu ya
wanasiasa na wengine watambua haki ni kama hisani au msaada au huruma
kutoka kwa viongozi.
Mathalan, ni kawaida kusikia wananchi wanaolipa
kodi wakiwaomba viongozi wao msaada wa kuwajengea barabara, zahanati,
shule na hata kuwaomba wawapeleke walimu katika shule zao.
Serikali inapofanya hivyo wananchi wanajua kuwa huo ndiyo msaada au uhisani kutoka kwa viongozi wao.
Bila kutambua kuwa viongozi au Serikali imetimiza
wajibu wake maana ipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi na ndio
maana inakusanya kodi.
Inawezekana kutokana na mtazamo huu finyu wa
kuziona haki za binadamu kama msaada au huruma ya viongozi kwa wananchi,
jamii kubwa imeshindwa kuzidai haki zake, imeshindwa kuzitambua haki
zake na wala kuzitetea haki zake.
Ndiyo maana enzi na enzi wananchi wengi wa nchi za
Kiafrika na hasa hapa Tanzania wamekuwa waoga hata kutoa maoni yao juu
ya matatizo au mafanikio waliyonayo.
Watafikwa na matatizo chekwa, lakini wataishia kulalama wajishindwa kusema japo ni haki yao.
إرسال تعليق