LEO yatupasa wote kumshukuru Mungu kutokana na kutuweka hai na tukiwa wazima wa afya, hakika ahimidiwe daima.
Nianze makala haya kwa kusema kuwa wakati pazia la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya mashine za kisasa za Biometric Voter Registration (BVR), likifunguliwa wiki iliyopita katika Jimbo la Kawe, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo sana sehemu mbalimbali jimboni humo.
Sambamba na hilo, kazi hiyo iliyotarajiwa kudumu kwa siku saba, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2015, ilianza kwa changamoto nyingine ya tatizo la kiufundi.Wakati safu hii ikiwa katika moja ya eneo ambako majaribio hayo yalikuwa yanafanyika, lilishuhudia wananchi wakiwa kwenye foleni kwa saa mbili baada ya mashine kugoma kuwaka.
Maofisa wa NEC waliokuwa wanasimamia kazi hiyo, walijitahidi kulishugulikia tatizo hilo, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda, hivyo kulazimika kuomba msaada kwa wataalamu wa masuala hayo (ICT), waliofika baada ya muda mfupi na kushughulikia tatizo hilo.
Tatizo hilo liliwashinda wasimamizi hapa Dar es Salaam, ikabidi waitwe wataalamu kutatua, nina wasiwasi kama tatizo hilo litatokea vijijini ambako hakuna wataalamu hao, naona kama linaweza kusababisha vurugu.
Nasema hivyo kwa sababu wananchi wataona kama vile wanahujumiwa wakati labda kweli ni tatizo la kiufundi.Labda Tume ya Taifa ya Uchaguzi ituhakikishie kuwa watalaamu hao wa ICT watakuwepo nchi nzima! Jambo ambalo nadhani litakuwa gumu sana.
Suala hilo la watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu linachangia wananchi kutojitokeza kwa kuona kuwa wanapoteza muda wao wa uzalishaji mali, hivyo ni lazima itafutwe mbinu ya kuhakikisha waandikishaji hawakai sana kwenye foleni ili kuepusha fujo na vurugu hasa siku za mwisho.
Lakini jambo linalonishangaza ni usemi kwamba Jimbo la Kawe linaanza kujaribiwa, kwa taarifa yenu ni kwamba mitaa mingi katika jimbo hilo zoezi hilo halipo. Kwa mfano Mlalakua Mwenge, Alhamisi iliyopita saa kumi na nusu nilifika, nikakuta ofisi imefungwa na zoezi hilo watu hawajui kama lipo.Ni wajibu wa viongozi wa vyama vya siasa kuwahamasisha wananchi kabla ya kuanza kwa kazi hiyo ya kuandikisha wananchi kwenye daftari.
Lakini navishangaa vyama vya siasa kwa kutohimiza wapiga kura kujiandikisha.
Naamini katika Manispaa ya Kinondoni ambako kulikuwa na zoezi la majaribio la uandikishaji kwa kutumia teknolojia ya mashine za kisasa za Biometric Voter Registration, wananchi wengi hawakupata nafasi ya kujiandikisha au kuhakiki.
Wakulaumiwa kwa hili ni wanasiasa kwa sababu mitaji yao ya kisiasa ni wapiga kura, sasa kama hawajiandikishi mambo yatakuwaje?Niiombe Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayosimamia zoezi hilo la uandikishaji kuongeza muda katika Jimbo la Kawe kwa sababu ni kweli wengi hawajajiandikisha.
Na kama wataacha kama ilivyo ambapo baadhi ya serikali za mitaa hazikufanya zoezi hilo kwa uzembe wa maofisa wa tume, tutarajie vurugu na malalamiko.Lakini kwa nini tufike huko na muda wa marekebisho upo?
Kwa asilimia kubwa waliosababisha uvurugwaji wa zoezi lile walikuwa wasimamizi wa uandikishaji na upigaji wa kura na ndiyo wanaopaswa kubeba lawama kwa fujo zote zilizotokea wakati wa shughuli hiyo.
Wiki iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia aliwasimamisha kazi wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali kutokana na kuchelewa kuandaa na kupeleka vifaa vya kupigia kura vituo vya kupigia kura jambo ambalo ni uzembe.
Uzembe huo ulijitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yao katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima wiki iliyopita.Waziri Ghasia anasema uamuzi huo umefanyika baada ya rais kwa mujibu wa sheria kuridhia adhabu hizo zitolewe.
Mambo ya uchaguzi siyo ya kuzembea au kuingiza itikadi za kisiasa, ni hatari kwa sababu nchi nyingi zinazoingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe chimbuko lake huwa kwenye kuwanyima haki wapiga kura.
Nasisitiza kuwa wananchi wa Jimbo la Kawe watakosa nafasi ya kupiga kura mwakani ikiwa itaonekana kuwa muda wa kujiandikisha umepita.Wangejiandikisha wapi wakati serikali za mitaa hasa ile iliyochukuliwa na wapinzani ilikuwa haifanyi kazi?
Ni lazima tume ya Taifa ya Uchaguzi ijifunze kutokana na chaguzi za hovyo za serikali za mitaa, iwaongezee muda watu wa Jimbo la Kawe, ili majaribio yao yaoneshe kama kweli mtindo huo unafaa au haufai.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
إرسال تعليق