Kasi ya Serikali kuwapatia askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) makazi bora na kuwarudisha kambini, ilishika moto jana,
Jumamosi, Desemba 20, 2014, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Amiri Jeshi Mkuu. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alipoweka jiwe la
msingi la ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya askari katika sherehe
hiliyofanyika Monduli, Arusha.
Nyumba hizo 6,064 za kubeba familia nane kila moja ni sehemu ya
nyumba10,000 za makazi ya wanajeshi zinazojengwa katika vikosi mbali mbali
vya JWTZ katika mikoa tisa ya Tanzania kwa gharama ya dola za Marekani
milioni 300.
Mradi wa kuwapatia wanajeshi makazi bora na kuwarudisha makambini ulianza
mwaka 2011, wakati Serikali ya Tanzania ilipopata mkopo wa ujenzi wa nyumba
hizo za wanajeshi ambako kati ya dola za Marekani milioni 300, Jamhuri ya
Watu wa China kupitia Benki ya China-Exim inatoa mkopo wa dola milioni 285
na Serikali ya Tanzania inatoa dola milioni 15.
Ujenzi wa nyumba hizo unaofanywa na Kampuni ya Shanghai Consturuction Group
General Company umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 50, ifikapo
Septemba mwaka 2017.
Mikoa tisa ambako nyumba hizo zinajengwa ni Arusha, Dar Es Salaam, Dodoma,
Kagera, Kigoma, Morogoro, Pemba, Pwani na Tanga na ni sehemu ya mpango
kabambe wa maboresho na uimarishaji wa JWTZ ambayo ni pamoja na kulipatia
Jeshi hilo zana za kisasa, vifaa bora zaidi, makazi mazuri, mafunzo na
huduma nyingine bora zaidi mbali mbali.
Akizungumza kabla ya kuweka rasmi jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba
hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo ni sehemu ya mpango
wa miaka 15 ya maboresho na uimarishaji wa JWTZ ambao hata hivyo, Serikali
yake imeamua kuutekeleza na kuukamilisha katika miaka saba tu.
إرسال تعليق