Maoni ya Katuni
Miaka minne iliyopita, Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kulizindua Bunge baada ya kuchaguliwa kipindi cha pili kuiongoza nchi yetu, miongoni mwa ahadi alizozitoa kwa wananchi ni kuboresha sekta ya elimu ikiwamo kuhakikisha shule zote za sekondari zinajengewa maabara za sayansi.
Katika kufuatilia ahadi zake, Agosti mwaka huu, akatoa tahadhari kwa viongozi ambao watashindwa kutekeleza agizo lake la ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya maabara tatu za masomo ya sayansi kwa kila shule, atachukua maamuzi mazito.
Akaagizo usimamizi wa ujenzi wa maabara kwa kila shule usimamiwe kwa karibu zaidi ili kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, kazi ambayo imeonekana kusuasua kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kiuchumi.
Hata hivyo, kwa kutambua gharama na mahitaji mengine ya kiutawala wakati wa kukamilisha kazi hiyo, Rais Kikwete ameongeza miezi sita ya kukamilisha ujenzi wa maabara hizo, baada ya muda wa miaka miwili alioutoa awali kumalizika tarehe 30 Novemba mwaka huu.
Alitoa agizo la operesheni ya ujenzi wa maabara baada ya kubaini kuwa ukosefu wa maabara kwa ajili ya masomo ya Fizikia, Kemia na Biolojia ilikuwa moja ya sababu za kuwakatisha tamaa wanafunzi nchini kupenda masomo ya sayansi.
Rais Kikwete amechukua uamuzi wa kuongeza muda zaidi ili kuwezesha kazi hiyo inayoendelea nchini kote kufanyika kwa usahihi, na maagizo hayo aliyatoa katikati ya wiki hii baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Arusha, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambaye pia ni Makamu wa Rais.
Kutokana na kuona umuhimu wa shule za sekondari kuwa na maabara zake, Rais alitangaza kwamba atachangia milioni 200/- katika Mfuko Maalumu wa Dhamana (Endowment Fund For Excellency) wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ambayo ni Taasisi ya pekee nchini.
Tathmini inaonyesha kuwa zipo idadi ya shule 3,463 ambazo zinahitaji maabara nchini, sawa na vyumba 10,389, lakini hadi kufikia Desemba 7 mwaka huu, vilikuwapo vyumba 3,867 vilivyokamilika ambavyo ni sawa na asilimia 37.2 .
Tunaamini kuwa kazi iliyobakia kukamilisha ujenzi huo bado ni nzito, inayohitaji kujituma na kujitolea kwa hali na mali, na hilo ni jukumu la wazazi wote wakishirikiana na viongozi katika maeneo yao. Aidha litakuwa jambo la kusikitisha endapo baadhi watajitokeza kubeza na kuwakatisha tamaa wananchi wengine katika jitihada za ujenzi wa maabara.
Ingawa ni asilimia 37.2 tu ya ukamilifu wa ujenzi huo hadi sasa, lakini hatua mbalimbali za ujenzi zimeendelea nchini kote na asilimia 56.7 ziko katika hatua nzuri za kukamilishwa, ingawa bado vyumba 631, sawa na asilimia 6.1 havijaanza kujengwa hadi sasa.
Bado tunaamini kazi kubwa imekamilika, eneo lililobakia litakamilishwa ndani ya miezi hiyo sita ya ziada.
Hata hivyo, Rais Kikwete alitoa pongezi za dhati kwa viongozi na wananchi nchini kote kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya hadi kufikia kiwango hicho.
Umuhimu wa kujenga maabara uliongezwa kasi kutokana na ongezeko kubwa la shule za sekondari, ambazo kwa mujibu wa Rais, zimeongezeka kutoka shule 828 mwaka 2004, hadi kufikia 3,551 kwa sasa.
Kwanza tunaipongeza serikali kwa kulivalia njuga suala la ujenzi wa maabara nchini, tukiamini dhamira hii itasaidia kuondokana na uhaba wa wataalamu katika fani mbalimbali za sayansi.
Tunatambua kuwa mwanzo huu ni mgumu lakini kwa vile nia ipo wazi, tutafikia hatua nzuri ya kutoa mafunzo ya sayansi na teknolojia mpya kwa usahihi zaidi.
Tunaamni kuwa kasi ya ujenzi wa maabara itakwenda vizuri na kukamilika katika kipindi cha miezi sita ambayo Rais ameongeza.
Ni rai yetu kwa wananchi huko vijijini kushirikiana na mamlaka zao ili kuhakikisha maazimio yaliyowekwa yanakamilika kwa faida ya watoto wetu pamoja na ustawi wa teknolojia ya sayansi nchini.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment