Dar/Songea. Tafrani ilizuka Dar es Salaam na
mjini Tunduru, mkoani Ruvuma, baada ya majambazi kuua mtu mmoja na
kupora zaidi ya Sh10 milioni katika matukio mawili tofauti.
Tukio la kwanza lilitokea jana katika eneo la
Morocco, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam ambako majambazi walipopora
Sh2 milioni kwa Nuru Patrick, huku mpita njia, Gloria Uroki akiuawa kwa
risasi.
Majambazi hayo yakiwa na silaha, yalipora mkoba
wenye fedha na wakati wanataka kukimbia, walianza kurusha risasi hovyo
na kusababisha kifo cha Uroki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa kumi jioni.
“Majambazi hao inaelekea walifahamu kuwa mwanamke
huyo ana fedha, kwa sababu aliposhuka tu kwenye daladala walimvamia na
kumpora mkoba,” alisema Wambura.
Katika tukio la Songea, watu wanaodaiwa kuwa ni
majambazi waliokuwa na bunduki aina ya SMG walimpora mfanyabiashara wa
madini raia wa Sri Lanka, Fadhiri Faiz (24) Sh8 milioni na simu tatu za
mkononi zenye thamani ya Sh1.8 milioni akiwa nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 1.40 usiku katika Mtaa wa
Misufini, Kata ya Mlingotini wilayani Tunduru.
Alisema kabla ya uporaji, majambazi hao walifyatua
risasi nne hewani na kumteka mlinzi wa Kampuni ya Wan Security, Hassan
Silaji (40), kisha wakavamia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.
إرسال تعليق