Doha, Qatar. Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Amina
Makilagi amesema kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni janja ya
Chadema kufifisha nguvu ya vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi.
Akizungumza katika mahojiano mafupi na gazeti hili
jana, Makilagi aliye katika ujumbe wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzuru
Falme za Kiarabu, alisema kwa sasa CUF na NCCR-Mageuzi havipo tena
kutokana na kumezwa na Chadema.
“Hawa Chadema ni wajanja, angalia walichopata wao
na hao CUF au NCCR Mageuzi. Ni ujanja ujanja tu, Chadema ndiyo
inayojitangaza,” alisema.
Alisema anabashiri mpasuko ndani ya Ukawa mwakani
kwa kuwa wapo waliojipanga kuwania ubunge na wanaweza kuenguliwa kwa
kusimamisha mtu mmoja wa upande mwingine.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema Ukawa walitumia nguvu nyingi na imeishia hapo, huku CCM ikiendelea kupeta.
Makilagi alisema kuwa wapinzani walitumia nguvu
nyingi katika maeneo mbalimbali ya mitaa nchini, lakini ushindi wa jumla
ni wa CCM.
Katibu Mkuu huyo wa UWT Taifa, alisema kuwa pamoja
na matokeo hayo ambayo CCM imepoteza baadhi ya mitaa, haoni wala
hadhani kama chama chake kimetikiswa kwani nguvu ya wapinzani imeishia
hapo na CCM inaendelea kupeta.
Alisema mtikisiko utatokea kwa umoja huo hasa
mwakani kwa wanaotaka kuwania ubunge, huku akisema kama CCM watajipanga
kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
“Unajua hapa watu wanaishi kwa malengo, sasa huoni
kila mahali, Chadema, kila mahali Chadema sasa hawa wengine kwani
hawataki?” alisema akihoji.
Alisema kuwa Chadema kinavifunika vyama vingine,
CUF na NLD na hiyo italeta mgongano ndani ya umoja huo na hasa
litakapokuja suala la posho.
Kuhusu mwelekeo wake kisiasa, alisema kuwa
kimsingi anajiandaa kisaikolojia kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma
Mjini, lakini endapo tu ataombwa kufanya hivyo. Makilagi alisema kuwa
kumekuwa na taarifa mbalimbali kuwa anatakiwa kuwania, lakini hiyo yote
itategemea na maombi ya Watanzania wengi.
“Niko huku Qatar, ninapata simu nyingi kuwa
wanataka niwanie ubunge mwakani, bado sijaamua, ninachofanya ni
kujiandaa kisaikolojia,” alisema- Mwananchi
إرسال تعليق