Maximo: Nawaangalia tu Yanga

???????????????????????????????
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM,
IKIWA ni siku tano sasa zimepita tangu Yanga kutangaza kuachana na Kocha Mbrazil Marcio Maximo, kocha huyo amesema anawaangalia na kuwasikiliza viongozi wa timu hiyo ambao hadi sasa hawajampa barua ya kuvunja mkataba wake.
Kwa sasa, Maximo yupo katika hali ya sintofahamu kutokana na wiki nzima hii magazeti mbalimbali kuripoti juu ya klabu ya Yanga kumtema bila kumpa barua yoyote mpaka sasa.
Kocha huyo aliyejizolea sifa wakati akiwa na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kabla heshima yake haijashuka Yanga, mpaka jana alikiri kutopewa barua ya kuvunja mkataba wake huo hivyo amebaki mguu ndani, nje.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu, Maximo alisema anatambua mchango wa wanahabari lakini amezuiwa kuongea lolote lile linalohusiana na yeye na Yanga ambao wamemtema.
“Napenda sana wanahabari na natambua mchango wao, ila siruhusiwi kuongea lolote cha zaidi mimi nawaangalia tu Yanga, nipo kimya siwezi kufanya chochote nikisubiri barua yangu ya kuvunja mkataba,” alisema kwa kifupi Maximo.
Hata hivyo, habari za ndani zilizopatikana jana zinaeleza kuwa, Yanga wameanza kupata hofu ya kumuacha kocha huyo kwa kile kilichodaiwa kuwa uamuzi huo utawagharimu kwa kiasi kikubwa, kwani Maximo amejiandaa na kuweka wanasheria watakaomsaidia katika suala hilo.
“Yanga mbali na kumlipa Maximo kama wakimuacha, uamuzi wao utawagharimu sana ndio maana hadi sasa hawajampatia barua ya kuvunja mkataba huo na wanajifikiria.
“Ukweli ni kama wanachemka, kwani katika akili ya kawaida hawakutakiwa kumfanyia hivyo Maximo, unaleta kocha mwingine wakati yeye bado yupo, gari inayombeba yeye ndiyo iliyokwenda kumpokea kocha mpya unafikiri na yeye hatajipanga, wangemalizana naye kwanza ndio wakamleta kocha mwingine.
Kocha anayetarajia kumrithi Maximo, Hans Van Der Pluijm juzi na jana jioni alitarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga, ili aweze kujua mustakabali wake.
Maximo ambaye bado anapenda kuifundisha Yanga, juzi na jana aliendelea na programu yake ya kuifundisha timu hiyo hadi hapo atakapoambiwa aache.
Kutupiwa virago Maximo kumekuja baada ya kukubali kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao Simba, katika mechi ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe iliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

- Mtanzania

Post a Comment

Previous Post Next Post