Dar es Salaam. Matokeo ya awali ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliofanyika nchi kote hivi karibuni yanaonyesha kuwa
wananchi wamebadilisha mitazamo yao dhidi ya vyama vya siasa na hivyo
kutoa picha mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Uchaguzi huo uligubikwa na malalamiko katika
baadhi ya maeneo nchini kiasi cha Serikali kuwaondoa kazini wakurugenzi
wa halmashauri tano kwa kushindwa kuusimamia vyema, pia umevipa vyama na
Serikali nafasi ya kujitafakari upya.
Kwa upande mmoja, uchaguzi huo umewapa nguvu
wapinzani kwa kuongeza idadi ya viti, lakini umeivuta nyuma CCM baada ya
kupoteza zaidi ya nafasi 2,600 za uenyekiti wa vijiji na mitaa
ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12,
042.
Vyama vya upinzani vimefanikiwa kuongeza kibindoni
viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika
mwaka 2009 ambapo vilipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Matokeo haya yametoa mwelekeo mpya kwa vyama vya
siasa nchini, wapinzani wakiamini huo ndiyo ufunguo wao kuelekea Ikulu
mwakani, CCM wakiamini kuwa huko ni kujikwaa tu na wataendelea kubaki
Ikulu mwakani kwani bado wanakubalika kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza mjini Dodoma hivi karibuni, Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda alisema
kwamba wakati CCM ikifanikiwa kupata ushindi wa jumla wa mitaa na vijiji
9,406, vyama vya upinzani vimepata nafasi 3,211.
Katika matokeo hayo CCM kimepata vijiji 7,290
kikifuatiwa na Chadema yenye vijiji 1,248. CUF imeshika nafasi ya tatu
kwa kuwa na vijiji 946, ikifuatiwa na UDP yenye vijiji vinne na TLP na
NLD vyenye viwili kila kimoja.
Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM kimechukua
jumla ya mitaa 2,116. vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni
Chadema (753), CUF (235), ACT (9), NCCR - Mageuzi (8) wakati vyama vya
TLP, UMD, UDP na NRA vimepata mtaa mmoja kila kimoja.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo nchini,
wananchi watapiga kura leo baada ya kushindwa kufanya hivyo Desemba 14
kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema matokeo hayo
ni dalili kuwa CCM itafanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.
Ingawa waziri huyo alikiri kuwa vyama vya upinzani
vimechukua maeneo mengi kuliko uchaguzi uliopita, alisema vyombo vya
habari vinatumika kupotosha hali halisi na kuifanya CCM kuonekana kuwa
imepoteza viti vingi kuliko uhalisia.
Matokeo hayo yanaonyesha CCM imepoteza viti zaidi
katika mikoa wa Dodoma, Lindi, Mtwara, Iringa, Arusha, Singida na katika
baadhi ya majimbo ya Dar es Salaam- Mwananchi
Post a Comment