Makilagi: Chadema ‘imeiua’ CUF, NCCR Uchaguzi Mitaa

Doha, Qatar. Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Amina Makilagi amesema kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni janja ya Chadema kufifisha nguvu ya vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi.
Akizungumza katika mahojiano mafupi na gazeti hili jana, Makilagi aliye katika ujumbe wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzuru Falme za Kiarabu, alisema kwa sasa CUF na NCCR-Mageuzi havipo tena kutokana na kumezwa na Chadema.
“Hawa Chadema ni wajanja, angalia walichopata wao na hao CUF au NCCR Mageuzi. Ni ujanja ujanja tu, Chadema ndiyo inayojitangaza,” alisema.
Alisema anabashiri mpasuko ndani ya Ukawa mwakani kwa kuwa wapo waliojipanga kuwania ubunge na wanaweza kuenguliwa kwa kusimamisha mtu mmoja wa upande mwingine.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema Ukawa walitumia nguvu nyingi na imeishia hapo, huku CCM ikiendelea kupeta.
Makilagi alisema kuwa wapinzani walitumia nguvu nyingi katika maeneo mbalimbali ya mitaa nchini, lakini ushindi wa jumla ni wa CCM.
Katibu Mkuu huyo wa UWT Taifa, alisema kuwa pamoja na matokeo hayo ambayo CCM imepoteza baadhi ya mitaa, haoni wala hadhani kama chama chake kimetikiswa kwani nguvu ya wapinzani imeishia hapo na CCM inaendelea kupeta.
Alisema mtikisiko utatokea kwa umoja huo hasa mwakani kwa wanaotaka kuwania ubunge, huku akisema kama CCM watajipanga kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
“Unajua hapa watu wanaishi kwa malengo, sasa huoni kila mahali, Chadema, kila mahali Chadema sasa hawa wengine kwani hawataki?” alisema akihoji.
Alisema kuwa Chadema kinavifunika vyama vingine, CUF na NLD na hiyo italeta mgongano ndani ya umoja huo na hasa litakapokuja suala la posho.
Kuhusu mwelekeo wake kisiasa, alisema kuwa kimsingi anajiandaa kisaikolojia kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini, lakini endapo tu ataombwa kufanya hivyo. Makilagi alisema kuwa kumekuwa na taarifa mbalimbali kuwa anatakiwa kuwania, lakini hiyo yote itategemea na maombi ya Watanzania wengi.
“Niko huku Qatar, ninapata simu nyingi kuwa wanataka niwanie ubunge mwakani, bado sijaamua, ninachofanya ni kujiandaa kisaikolojia,” alisema
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post