Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
Aliiambia NIPASHE kuwa mara kwa mara amekuwa akikutana na wadau wa vyama vya siasa kwa ajili ya kuwahamasisha kufanya siasa za kistaarabu.
Alisema matukio yaliyojitokeza katika uchaguzi wa serikali ya mtaa ofisi yake itayasimamia ili yasijitokeze katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Yale ambayo yamejitokeza katika sheria yatafanyiwa kazi kwa sasa, hivyo dosari hizo ni bora zilivyojitokeza mapema ili zifanyiwe kazi zisijitokeze katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Jaji Mutungi alisema panapotokea vurugu katika uchaguzi haina maana kuwa chama pekee kinapata hasara kwa kuwa wanaoumia ni Watanzania.
Alisema kuna haja ya kuelimishana maana ya ustaarabu, kuheshimiana na kuaminiana ili watu waelewe kwa upana.
Alisema Tanzania haina historia ya fujo ama vurugu katika siasa na kwamba mambo hayo yanaigwa kutoka kwa mataifa mengine.
“Kuna nchi zinahangaika kujua ni namna gani Tanzania inafanya uchaguzi kwa amani, huwa wanatoka nchini kwao na kuja kuangalia jinsi tunavyoendesha uchaguzi wa wetu halafu leo hii kunatokea fujo,” alisema.
Aliongeza: “Lakini kwa sasa napata wasiwasi tunapokwenda hii sifa inataka kuondoka.”
Jaji Mutungi alisema suala la amani siyo la ofisi yake wala Tume ya Uchaguzi ni jambo la Watanzania wote, hivyo ni muhimu kuwapo kwa ustaarabu katika siasa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment