Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Saada aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa takwimu za pato la taifa zilizorekebishwa kwa Tanzania Bara.
Alisema ikilinganishwa na Sh. trilioni 20.9 ambazo ni takwimu za pato la Taifa zilizokuwa zinatumia bei za bidhaa na huduma za mwaka 2001 sasa limeongezeka.
“Hii ni sawa na ongezeko la ukubwa wa pato la taifa kwa kiasi cha asilimia 27.8, wastani wa pato la mwananchi mwaka 2013,” alisema.
“Kwa kutumia takwimu za pato la taifa zilizorekebishwa ni Sh. milioni 1.6 ambazo ni sawa na dola za Kimarekani 977 ikilinganishwa na Sh. milioni 1.8 kwa kutumia pato la taifa za bei ya mwaka 2001,” alisema.
Alisema ukuaji wa uchumi umechangiwa na shughuli za kukua kwa Sayansi na Teknolojia ambapo utumiaji wa simu za kiganjani umeongezeka.
Aidha, alisema ujenzi wa miundombinu umesaidia utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi huku sekta ya kilimo zao la nyanya limeongezeka thamani katika pato la taifa.
“Serikali na sekta binafsi zimeweza kuongeza ajira mpya zipatazo 400,000 kati ya 600,000 zilizokuwa zinatarajiwa, pia huduma za upatikanaji wa maji safi na salama zimeendelea kuimarika sasa zaidi ya asilimia 60 ya kaya zinazopata huduma hii,” alisema.
Saada alisema mchango wa pato la taifa kwa shughuli kuu za kiuchumi kwa bei ya mwaka 2013 ilikuwa Sh. trilioni 69.8 wakati wastani wa pato kwa kila mtu ni Sh. milioni 1.6.
“Shughuli za kiuchumi za huduma zina mgawo mkubwa zaidi ya pato la taifa wa asilimia 43.7 wakati viwanda na ujenzi vina mgawo wa takribani ya asilimia 22.7,” alisema.
Aidha, amewataka maafisa na wadau mbalimbali kutumia takwimu hizo kwa ajili ya maendeleo. Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa, alisema takwimu hizo ni shirikishi na kwamba ni bora zaidi katika kufuatilia sera za uchumi jumla na nyingine kwa kuwa zimeboreshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Alisema wataziweka kwenye tovuti ya NBS kwa ajili ya kupanua wigo mpana wa matumizi yake ndani na nje ya nchi huku elimu kwa umma ikiendelea kutolewa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment