Karatu. Waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro akiwamo aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo
ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Bernard Mrunya
wamepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Karatu kujibu
tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka
wakati wakiwa watumishi katika mamlaka hiyo.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni washtakiwa
watano, mbali ya Mrunya, wengine ni Leornard Minzi aliyekuwa Mkuu wa
Kitengo cha Ununuzi na Victor Appolo aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ikolojia
Wengine ambao mpaka sasa ni watumishi katika
mamlaka hiyo ni Bruno Kawasange, Mkurugenzi wa Hifadhi na Maendeleo ya
Jamii na Justice Muumba, Meneja wa Maendeleo ya Jamii.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi
wa Mahakama ya Wilaya, Ally Mkama, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hamidu Sindano akishirikiana
na Richard Jacopiyo.
Waliieleza Mahakama kuwa katika tarehe tofauti
kati ya Aprili na Februari, 2011 na 2012, washtakiwa walitumia madaraka
yao vibaya kwa kushawishi kumpa kazi mtaalamu mshauri, Michel Duplat
raia wa Ufaransa bila kufuata utaratibu ulioelekezwa na Sheria za
Ununuzi ya Umma ya Mwaka 2004, kitendo kilichosababisha Duplat kulipwa
fedha za umma kinyume na utaratibu.
Washtakiwa kwa pamoja walikana mashtaka
yanayowakabili, hawakutakiwa kuzungumza chochote mahakamani hapo na
waliachiwa kwa dhamana na wakiamriwa kutosafiri nje ya nchi.
Kesi hiyo iliahirishwa na itatajwa tena Januari 6, mwakani kwa kuendelea kusikilizwa.
إرسال تعليق