Ngara. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera imewataka
wamiliki wa pikipiki kuhakikisha wanasajili vyombo hivyo kwa muda
unaotakiwa, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Ofisa Elimu kwa Walipa Kodi Mkoa wa Kagera, Simon
Masawe alisema juzi kuwa idadi ya pikipiki zilizosajiliwa ni 859 ambazo
ni ndogo ukilinganisha na wingi wa pikipiki.
Alisema wamiliki wanatakiwa kuhakikisha
wanazisajili kabla usajili wa kufanya msako kila wilaya, utakaowahusu
wale waliokiuka taratibu haujafuatwa.
Alisema Serikali imeamua kusajili namba za pikipiki ili kurahisisha usimamizi na utawala wa vyombo hivyo tangu Oktoba mwaka huu.
“Ili kufanikiwa zoezi hili, imetolewa miezi sita
kwa kila mmiliki wa pikipiki kuisajili kwa kuzingatia maelekezo ya
mameneja wetu kila wilaya,” alisema Masawe.
Alisema waendesha pikipiki maarufu kwa jina la
Bodaboda wameitaka Serikali kuruhusu TRA kufanya usajili huo katika
wilaya zao, ili kumaliza kazi hiyo mapema.
Mwendesha bodaboda, Edson William alisema TRA
inatakiwa kusogeza huduma ya usajili karibu na walengwa ili kuepusha
gharama za kusafiri kwenda makao makuu ya mkoa iliyopo Manispaa ya
Bukoba.
William alisema pamoja na usajili bado waendesha
pikipiki na wamiliki wao hawajapewa elimu ya usajili na matumizi ya
vyombo hivyo.
Alisema kitendo cha kuelekezwa kwenda kusajili
pikipiki mkoani, baadhi ya bodaboda watakosa kufanya kazi kwani
wanategemea wamiliki ndiyo wasajili na wao wafanye kazi na kuwasilisha
mapato.
Post a Comment