TRA: Pikipiki zisajiliwe kwa muda uliowekwa

Ngara. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera imewataka wamiliki wa pikipiki kuhakikisha wanasajili vyombo hivyo kwa muda unaotakiwa, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Ofisa Elimu kwa Walipa Kodi Mkoa wa Kagera, Simon Masawe alisema juzi kuwa idadi ya pikipiki zilizosajiliwa ni 859 ambazo ni ndogo ukilinganisha na wingi wa pikipiki.
Alisema wamiliki wanatakiwa kuhakikisha wanazisajili kabla usajili wa kufanya msako kila wilaya, utakaowahusu wale waliokiuka taratibu haujafuatwa.
Alisema Serikali imeamua kusajili namba za pikipiki ili kurahisisha usimamizi na utawala wa vyombo hivyo tangu Oktoba mwaka huu.
“Ili kufanikiwa zoezi hili, imetolewa miezi sita kwa kila mmiliki wa pikipiki kuisajili kwa kuzingatia maelekezo ya mameneja wetu kila wilaya,” alisema Masawe.
Alisema waendesha pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda wameitaka Serikali kuruhusu TRA kufanya usajili huo katika wilaya zao, ili kumaliza kazi hiyo mapema.
Mwendesha bodaboda, Edson William alisema TRA inatakiwa kusogeza huduma ya usajili karibu na walengwa ili kuepusha gharama za kusafiri kwenda makao makuu ya mkoa iliyopo Manispaa ya Bukoba.
William alisema pamoja na usajili bado waendesha pikipiki na wamiliki wao hawajapewa elimu ya usajili na matumizi ya vyombo hivyo.
Alisema kitendo cha kuelekezwa kwenda kusajili pikipiki mkoani, baadhi ya bodaboda watakosa kufanya kazi kwani wanategemea wamiliki ndiyo wasajili na wao wafanye kazi na kuwasilisha mapato.

Post a Comment

أحدث أقدم