Morogoro. Wanawake 14 na wanaume wawili wamehukumiwa kifungo cha
nje cha miezi mitatu kwa makosa ya kufanya biashara ya ngono katika
maeneo mbalimbali.
Kukamatwa kwa watu hao kulitokana na Jeshi la Polisi kufanya msako katika maeneo ya Kahumba na Itigi Masamvu.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard
Paulo alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu za Sikukuu za Krismasi
na Mwaka Mpya kwa wananchi wa mkoani hapa.
Alisema wafanyabiashara hao wa ngono pia wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya wizi na uhalifu mwingine.
Kamanda Paulo alisema polisi wamejipanga
kukabiliana na uhalifu na vitendo vya kuvunja amani vitakavyojitokeza
wakati wa sikukuu hizo.
Alisema kuwa watu hao maarufu kwa biashara ya uchangudoa na ukahaba, walikamatwa Desemba 21 mwaka huu saa 6:00 usiku.
Alisema siku iliyofuata walifikishwa mahamani na
kukiri shtaka na hivyo kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu ili
iwefundisho kwa wengine.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Paulo alisema
wataendelea kufanya msako huo katika maeneo mbalimbali ili kukomesha
biashara hiyo haramu.
Pia, alisema kuwa polisi watafanya doria kwa
miguu, magari pamoja na mbwa katika nyumba za ibada, kwenye mikusanyiko
ya watu ikiwamo Kituo cha Mabasi cha Msamvu na barabara kuu zinazokatiza
Morogoro kuelekea mikoa mingine.
Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha dhana ya ulinzi jirani na ukamataji salama inazingatiwa.
Aliwakumbusha wananchi kuziacha nyumba zao zikiwa na ulinzi wa uhakika katika kipindi cha sikukuu.
Kamanda alisema hata wale wenye vyombo vya usafiri
hasa magari wanapaswa kuhakikisha wanavifunga kabla ya kwenda kwenye
nyumba za ibada.
إرسال تعليق