Waislamu wampongeza JK kumtimua Tibaijuka

Waislamu  wa madhehebu ya Shia nchini wamempongeza Rais  Jakaya Kikwete kwa kumtimua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka pamoja na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kupisha uchunguzi kuhusu sakata la  akaunti  ya Tegeta Escrow.
Pongezi hizo zimetolewa Jana na Imamu wa Msikiti wa Mashia wa Kigogo, Dar es Salaam, Sheikh Hemed Jalala , wakati akitoa  salamu za sikukuu ya Krismas kwa Wakristo nchini na Duniani nakuwatakia kheri ya Mwaka Mpya wa 2015.

Alisema lengo la salamu hizo ni kuonyesha kuwa waumini wa dini ya Kiislamu na Wakristo wapo pamoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo na furaha.

“Waislamu  wana  itikadi zao pia Wakristo, hivyo hivyo, kinachotuunganisha sisi ni utaifa tulionao ambao unapelekea kuvumiliana katika mambo mengi,” alisema Shekhe Jalala.

Alisema Serikali inapaswa kuwaangalia kwa karibu viongozi wa dini  zote nchini  kama ni watu ambao wataendeleza umoja uliopo na  kudumisha amani iliyopo.

“Endapo amani na umoja vikitoweka nchini hakuna kiongozi wa dini  ambaye  ataweza kukaa katika nyumba ya ibada na kuhubiri amani tena kama ilivyo sasa ,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post