Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF)
kimesema, hakitarudi nyuma na kitaendelea kufanya maandamano na mikutano
ya hadhara kila Januari 26 na 27 kila mwaka kuazimisha mauaji ya
wanachama wake yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.
Katika maadhimisho yaliyofanyika mwaka huu,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 32 wa chama
hicho walipigwa kisha kushikiriwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya
kuendesha maandamano yasiyokuwa na kibali.
Kutokana na kosa hilo, jana Profesa Lipumba
alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa na
kusomewa shtaka la kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la
jinai.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa
leo, Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Juma Duni Haji alisema hakuna ubaya
wowote kuwaenzi na kuwakumbuka wapendwa wao kwa kufanya mikutano na
maandamano.
“Jeshi la Polisi linatakiwa kutambua ya kwamba
kila Januari 26 na 27 tutaendelea kufanya mikutano na maandamano, kama
hawataki kuelewa hilo wakae mkao wa mapambano na wananchi kila mwaka.”
“Nadhani maadhimisho ya Januari 26 na 27 mwaka
2016 yatakuwa makubwa zaidi kulingana na Jeshi la Polisi
litakavyokabiliana nayo,” alisema Haji
Aliongeza: “Jeshi la Polisi limekosa maadili
halifai, linahitaji marekebisho makubwa na tunamtaka Rais (Jakaya
Kikwete) kuwawajibisha wahusika wote wa tukio hili-viongozi wa Jeshi la
Polisi.”
Haji alisema, “Tunalaani kupigwa kwa viongozi na
wafuasi wa Chama chetu na Jeshi la Polisi na tunalitaka kutekeleza
majukumu yake kwa kutumia weledi na kuacha ushabiki na kutumiwa kisiasa
kwa visingizio vya kiitelinjensia.”
Kuhusu afya ya Profesa Lipumba, Mkurugenzi wa
Fedha wa CUF, Joran Bashange alisema, “Profesa Lipumba Manaendelea
vizuri na kwa ushauri wa daktari amemwambia apumzike kwa siku tatu bila
kufanya kazi ya aina yoyote.”
Aliongeza: “Mwenyekiti (Lipumba) hana maradhi ya
shinikizo la damu lakini kutokana na kadhia hiyo ndiyo iliyosababisha
yeye kupata shinikizo hilo kwani alipokamatwa alitumia saa 6 kuhojiwa na
polisi waliokuwa wakibadilishana mahojiano yaliyofikia hatamu saa 6
usiku.”
Post a Comment