Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo amebanwa bungeni kuhusu
mkanganyiko uliopo katika mpango wa uandikishwaji wa daftari la
wapigakura kutumia mashine za BVR na mgogoro uliopo kati ya Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa(Nida) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec) kuhusu
vitambulisho vya kupigia kura.
Katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni
leo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe alimtaka Pinda
kueleza Serikali ina mpango gani kuhakikisha hakuna tatizo litakalotokea
katika uandikishaji wa daftari hasa ikizingatiwa muda uliopo hautoshi
na majaribio ya uandikishaji kwa BVR umeibua kasoro nyingi.
Mbowe alisema majaribio ya uandikishaji wa kutumia
BVR katika jimbo la Kawe, Wilaya ya Mlele na Kilombero yameibuka na
changamoto mbalimbali na huku nchi ikitakiwa kuandikisha wapigakura
zaidi ya milioni 24.
Pia alitaka kujua kama muda uliopangwa wa uandikishaji unatosha ikizingatiwa zimebaki siku 90 kufikia kwenye kura ya maoni.
Akijibu swali hilo Pinda alisema: “Aliyoyasema
Mbowe Serikali haiwezi kuyapuuza hata kidogo na ni kweli mchakato huo
umekuwa na matatizo kidogo hasa ya fedha na Serikali imekuwa ikipambana
ili kuweza kufanikisha mchakato huo.
“Tatakwenda na ratiba kama Tume ilivyopanga na
nakubaliana na Mbowe kwamba lazima kuwe na ushirikishwaji hasa wa
vyama,”alisema Pinda.
Alisema kuwa BVR 250 zilizoingia kwa ajili ya
majaribio ilikuwa ni za kupima uwezo wake na kweli kuna matatizo ya hapa
na pale ambayo yanashughulikiwa ili yasiwepo wakati zoezi rasmi
litakapoanza rasmi na kuweza kufika salama kwenye uchaguzi mkuu.
Akijibu suala la muda kutokutosha uandikishaji wa
daftari hilo Pinda alisema kama ikitokea Nec ikitaka muda uongezwe basi
atawasilisha suala hilo bungeni.
Alisema mashine za BVR kwa taarifa alizopewa na
Nec ni kwamba moja inaandikisha watu 70 kwa siku moja na siyo 22 kama
alivyosema Mbowe.
Post a Comment