Dar es Salaam. Wakati wafuasi 30 wa CUF jana walifikishwa mbele
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya
kula njama, kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano bila ya
kibali, chama hicho kimesema kitaendelea kuenzi siku ya kukumbuka wenzao
waliofariki wakati wa machafuko Zanzibar mwaka 2001.
CUF ilitoa tamko la kuendelea na maandamano na
mikutano ya hadhara jana kwenye mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho na baadaye alasiri
wafuasi hao 32 walifikishwa mahakama kwa mashtaka hayo matatu yanayohusu
maandamano ya kuadhimisha mauaji ya wenzao waliokuwa wakipinga matokeo
ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2000.
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo alidai katika
shtaka la kwanza kuwa washtakiwa walikula njama za kufanya uhalifu
Januari 27,2015 wakiwa Temeke na kwamba katika shtaka la pili washtakiwa
28 kati ya 30 walikusanyika isivyo halali kwenye ofisi ya CUF karibu na
Hospitali ya Wilaya ya Temeke na kufanya maandamano kuelekea Zakhem,
Mbagala.
Katika shtaka la tatu, ambalo nalo pia
linawakabili washtakiwa 28, inadaiwa siku hiyo hiyo, wakiwa eneo la
Mtoni Mtongani waligoma na kutojali tangazo halali la polisi la kuwazuia
kuandamana na kukusanyika.
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni
Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma
Mattar (54), Muhamed Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji
Mohamed(39), Abdul Juma(40), Hassan Said (37), Hemed Joho (46) na
Mohamed Ibrahim (31).
Wengine ni Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi
Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma
(33), Salehe Ally (43), Abd Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah
Ally(32) , Said Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25),
Abdallah Said(45),Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said
(39).
Washtakiwa Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37) hawahusiki katika shtaka la pili na tatu.
Washtakiwa hao kwa pamoja walikana mashtaka yote
na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika. Hakimu Emilius Mchauru, ambaye aliahirisha kesi hiyo hadi
leo, alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini
dhamana ya Sh 100,000. Hata hivyo, washtakiwa hao wamepelekwa mahabusu
hadi leo ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kukagua barua za
wadhamini.
Naye Ibrahim Yamola anaripoti kuwa CUF imesema
itaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kila ifikapo
Januari 26 na 27 kuadhimisha mauaji ya wanachama wake.
Maadhimisho ya mwaka huu yalizuiwa na Jeshi la Polisi.
Makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji, ambaye
pia aliingia matatizoni wakati wa machafuko hayo ya mwaka 2001, alisema
hakuna ubaya wowote kuwaenzi na kuwakumbuka wapendwa wao.
“Jeshi la Polisi linatakiwa kutambua kwamba kila
Januari 26 na 27 tutaendelea kufanya mikutano na maandamano, kama
hawataki kuelewa hilo, wakae mkao wa mapambano na wananchi kila mwaka,”
alisema Haji.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق