Esther Matiko ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara. Ni mmoja wa wanasiasa vijana anayebeba matumaini ya vijana wengi nchini.
Kwa kutambua mchango wake hasa kwa kushiriki
kikamilifu katika mijadala mingi ya Bunge, makala hii leo inamulika
historia ya maisha yake na kugusia baadhi ya mambo muhimu aliyokutana
nayo katika maisha yake ya kisasa.
Swali: Nani aliyekushawishi kuingia katika siasa?
Jibu: Siasa ni fursa ya utumishi. Ni eneo mojawapo
unalopata fursa ya kuitumikia jamii na Taifa kwa ujumla. Kuhusu
ushawishi ulianzia ndani ya familia, kwani baba yangu pamoja ya kuwa
mwajiriwa alipenda siasa na kushiriki kwa kiwango kikubwa.
Lakini pia nje ya familia kuna wanasiasa
walionivutia akiwamo marehemu Chacha Wangwe na kunifanya nihisi kupitia
siasa nitawatumikia na kuwasemea wanyonge na maskini pamoja na kutetea
rasilimali za nchi yangu.
Swali: Je, ulijisikiaje siku ya kwanza ulipoingia bungeni ukiwa Mbunge? Nani aliyekuwa mwenyeji wako siku hiyo?
Jibu: Kwanza sikuamini hadi pale niliposimama
mbele ya spika na kula kiapo cha ubunge. Kiukweli ile siku sitoisahau
kwani niliona ile ndoto yangu ya siku nyingi ya kuwasemea wananchi wa
Tarime na kuwa kiongozi wa kisiasa wa kitaifa imeanza kutimia.
Swali: Kwa kipindi chote ambacho umekuwa bungeni ni siku gani ambayo hutoisahau? Na kwa nini?
Jibu: Yapo matukio mengi ambayo sitoyasahau,
lakini mojawapo ni mchakato wa kupata wawakilishi wa wabunge katika
Mabaraza ya Vyuo Vikuu.
Niliomba nafasi ya kuliwakilisha Bunge kwenye
Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) na nakumbuka hadi muda wa
ukomo wa kurudisha fomu nilikuwa peke yangu niliyekuwa nimerudisha fomu,
lakini cha kusikitisha ni kwamba siku ya kupigiwa kura nikaona jina la
mbunge mmoja mwanamke wa CCM nalo likitajwa licha ya kwamba hakuwa
ameomba nafasi hiyo, kutokana na hali hiyo niliamua kujitoa kwa sababu
tayari niliona kuna mazingira yasiyokuwa ya haki.
Swali: Wewe ni Mbunge wa Viti Maalumu je, kipi umekifanya tangu ulipopata wadhifa huu?
Jibu: Nimefanya mambo mengi sana, nimesaidia
makundi mbalimbali ya vijana, wanawake, wazee na watoto katika
kuwajengea uwezo wa kiuchumi, michezo, msaada wa kisheria na mengineyo- Mwananchi
إرسال تعليق