Mabomu yaliyofatuliwa na Jeshi la Polisi Jumanne
wiki hii kuwazuia wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF),
wasifanywe maandamano yaliwaathiri watoto wa shule ya awali ya Mango
(Madrasat Munawara), iliyopo Mtoni Mtongani, Temeke, Dar es Salaam.
Mwalimu wa shule hiyo, Nasra Mohamed, alisema hakuna mtoto
aliyepotea kutokana na tukio la mabomu, lakini moshi wa mabomu
uliwachanganya na kukimbia ovyo.
Alisema watoto wote walikimbilia nyumbani kwao, lakini walipoteza
vitu mbalimbali walipokuwa wakikimbia ili kunusuru maisha yao kutokana
na mabomu yakiyokuwa yakipigwa mfululizo.
“Mimi mwenye nilikuwa nalia kama mtoto mdogo ili kuwanusuru
wanafunzi wangu, nilinawa maji ya kuoshea chipsi, lakini kama
nisingepata maji hayo hali ilikuwa mbaya sana kwangu,” alisema.
Nasra alisema wakati mabomu hayo yanapigwa alikuwa kwenye kibanda
cha chipsi, hivyo alimwona askari mmoja akiwa kwenye makutano ya
barabara ya Mtongani akipiga mabomu mfululizo, kitendo kilichofanya
akimbie haraka hadi shuleni kuwahi wanafunzi.
Alisema alipofika alikuta watoto wote wanakohoa na kutupa viti vyao mbalimbali na kukimbia hovyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtongani, Khamis Mtonga, alisema Serikali
haikupaswa kutumia nguvu kubwa katika kuzuia maandamano bali hekima na
busara ilipaswa kuzingatiwa kuhakikisha usalama wa raia unaimarishwa
kwenye mkutano huo.
Mtonga alisema kuwa taharuki hiyo ilisababisha baadhi ya watu wasio
na hatia, wakiwamo watoto kukimbia hovyo kwa nia ya kuokoa usalama wao.
“Bado sijapata taarifa ya mtoto au mtu mzima aliyepata madhara
kutokana na milipuko ya mabomu hayo bali ilikuwa patashika mtaani,”
alisema.
Wanachama, wapenzi na viongozi wa CUF akiwamo Mwenyekiti wake wa
Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba walipigwa mabomu na kukamatwa na polisi
wakidaiwa kutaka kuandamana bila kibali.
Wanachama hao walikuwa wameandaa maandamano kutoka ofisi za CUF
Wilaya ya Temeke hadi viwanja vya Zamkhen, Mbagala kwa ajili ya mkutano
wa hadhara.
Lengo na maandamano na mkutano huo lilikuwa ni kumbukumbu ya miaka
14 ya wenzao zaidi ya 30 waliouawa na Jeshi la Polisi mwaka 2001 wakati
wakipinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar wa mwaka 200.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق