Magaidi washambulia hoteli,Libya

Hoteli ya Corinthia iliyoshambuliwa na magaidi
Watu wenye silaha wamevamia Hoteli ya hadhi ya juu mjini Tripoli nchini Libya kisha kutega bomu kwenye gari nje ya Hoteli hiyo.Mitandao ya kijamii yenye uhusiano na kundi la wapiganaji wa IS nchini humo imesema kuwa wametekeleza shambulio hilo.
Vyanzo vya usalama nchini Libya vinasema takriban walinzi watatu wa Hoteli hiyo waliuawa katika shambulio hilo, sambamba na Raia kadhaa wa kigeni.Vyanzo hivyo vimesema kuwa baada ya tukio hilo Watu hao wenye silaha walijilipua kwa mabomu.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Jane Psaki amekemea tukio hilo, na kusema kuwa kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa kuwa miongoni mwa waliouawa ni Raia wa Marekani. Amesema wanakemea shambulio la kigaidi katika hoteli ya Corinthia mjini Tripoli, wanatuma salamu za rambirambi kwa waathirika na familia zao,wanaendelea kuwa imara katika msimamo wao wa kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa kuwasaidia raia wa Libya kuunda serikali yenye mfumo shirikishi.
Jane amefafanua kuwa machafuko hayawezi kuondoa matatizo ya Libya na shambulio hili haliwezi kuwa kikwazo kwa mchakato wa kutafuta suluhu ya kisiasa.(BBC)

Post a Comment

Previous Post Next Post