Matukio ya uporaji silaha yameendelea kuliandama
Jeshi la Polisi nchini baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi
kuwapora askari wake bunduki mbili aina ya SMG kisha kumjeruhi kwa
kumchona kisu mmoja wao.
Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana katika Jiji la Tanga,
pia lilihusisha uporaji wa risasi kutoka kwa walinzi hao wa usalama wa
raia na mali zao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, akizungumza na
NIPASHE, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 5:15 usiku katika
eneo la barabara ya tano mjini Tanga.
Kamanda Ndaki alisema katika tukio hilo, askari mmoja PC Masoul
alichomwa kisu na amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bomba
kwa matibabu.
Alisema askari huyo alipata mkasa huo wakati akiwa na mwenzake PC
Mwalimu wakiwa katika doria mjini Tanga na ghafla walivamiwa na watu
ambao wanasadikiwa kuwa majambazi kisha kuwapora bunduki hizo.
“Tumeanza upelelezi wa tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu
aliyekamatwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pia imekaa kujadili
tukio hlo,” alisema Ndaki.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa askari hao
waliporwa silaha hizo walipokwenda kula chips katika eneo hilo na baada
ya kumaliza walipoanza kuondoka ndipo walipovamiwa na majambazi .
Chanzo chetu cha habari kinaeleza kwamba kabla ya kuporwa bunduki
hizo askari hao walipigwa ili kuwashinikiza kukubali kuziachia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fresser Kashai, alipotafutwa kutoa
maelezo zaidi kuhusiana na tukio hilo, alisema yuko nje ya mkoa. Kashai
anahudhuria mkutano wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi mjini
Dodoma uliofunguliwa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku saba tu tangu majambazi
walipokivamia kituo cha polisi Ikwiriri wilayani Rufiji, mkoani Pwani
na kuwaua askari wawili na kuiba bunduki saba.
Katika tukio hilo, majambazi hao ambao walidaiwa kuwa zaidi ya 10
waliiba bunduki aina ya SMG mbili, SAR mbili, Shortgun moja na bunduki
mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
Askari waliouawa ni PC Judith Timoth na Koplo Edga Mlinga, hadi
sasa Jeshi la Polisi halijatoa maelezo kuhusiana na msako unaoendelea
kama kuna watuhumiwa waliokamatwa, licha ya Mkuu wa Jeshi hilo (IGP),
Ernest Mangu, kutangaza bingo ya Sh. milioni 20 kwa mtu atakayetoa
taarifa zitakazowezesha kuwatia mbaroni waliohusika.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment