Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameanza kukumbana
na changamoto za wizara hiyo baada ya kukutana na wasafirishaji wa
wawili wa dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) waliokuwa na kete zaidi 154 aina ya Heroine zenye thamani
ya mamilioni ya fedha kwenda nje ya nchi.
Sitta alikutana na wauza ‘unga’ hao ikiwa ni ziara yake ya kwanza
tangu Rais Jakaya Kikwete alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na
kumteua kuwa Waziri wa Uchukuzi akibadilishana na Dk.Harrison Mwakyembe
ambaye amehamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Watuhumiwa hao ambao Sitta alikutana nao katika uwanja huo wakiwa
chini ya ulinzi wa maofisa wa uwanja huo ambao wote ni raia wa Tanzania
ni wanawake (33), mkazi wa Sinza na wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wanawake hao alikuwa na hati ya kusafiria namba AB 651920
wakati mwingine alikuwa na hati ya kusafiria namba AB 636250,
walikamatwa Januari 23, mwaka huu saa 5:15 usiku wakitaka kusafiri kwa
ndege ya shirika la Emirate.
Watuhumiwa hao ambao kila mmoja ilielezwa alikuwa amemeza tumboni kete 77 za dawa hizo.
Waziri Sitta alipowahoji walimweleza kuwa walitumwa na mtu mmoja
ambaye hawakumtaja jina ila walikuwa na namba yake ya simu ili
wazisafirishe kwenda Hong Kong kwa malipo ya Dola za Marekani 6,500.
Kufuatia hali hiyo,Sitta aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama
kuwahoji zaidi watuhumiwa hao ili kuweza kubaini mtandao na kuwachukulia
hatua wahusika na kwamba serikali haitaki kuona viwanja vya ndege hapa
nchini vinakuwa kichochoro cha kupitishia dawa hizo.
Alisema serikali haitamuonea haya mfanyakazi yeyote wa viwanja vya
ndege nchini atakayebainika kushiriki kula njama kufanikisha kusafirisha
dawa za kulevya na kwamba atakayekamatwa mbali na kusimamishwa kazi pia
atawekwa ndani kusubiri uchunguzi ufanyike kabla ya suala lake
kupelekwa mahakamani.
WALIOFANYA SHEREHE BANDARINI WAONYWA
Katika hatua nyingine, Waziri Sitta, ametuma salamu kwa wafanyakazi
wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambao wanadaiwa kufanya sherehe
baada ya kuhamishwa Dk. Mwakyembe katika wizara hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa TPA wanadaiwa kufanya sherehe kuhamishwa
kwa Dk.Mwakyembe katika wizara ya Uchukuzi na kwamba ujio wa Sitta
itakuwa mteremko kwao kuendelea na vitendo vya wizi kama ilivyokuwa
awali kwa madai waziri Sitta hataweza kuwathibiti kama ilivyokuwa
Mwakyembe.
"Nimepata taarifa kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Bandari walifanya
sherehe baada ya kusikia Dk. Mwakyembe amehamishwa katika wizara hii ya
Uchukuzi, kicheko chao kitakuwa kilio chao na kina mwisho, waliodhani
maji yamepoa wanajidanganya kwa kuwa maji sasa ndiyo yamechemka"
alisema.
UCHUMI UPO KICHWA CHINI MIGUU JUU
Waziri Sitta akiwa katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(Tazara) alisema ni jambo la kushangaza kuona wakati nchi ina mtandao wa
barabara zaidi ya kilometa 2000 na mizigo ya kusafirisha ipo lakini
kila iku tunatembeza bakuli kuomba China.
"Uchumi wetu hivi sasa upo kichwa chini miguu juu,tunasafirisha
mizigo kupitia barabara na barabara zinaharibika wakati baadhi ya mizigo
tungeweza kusafirisha kwa reli,"alisema.
Aliongeza kuwa kila siku Waafrika wanachekwa na kwa bra serikali
imejipanga kuhakikisha miundombinu ya reli inaboreshwa na kujenga reli
mpya katika maeneo mbali mbali ili usafiri huo uwe wa uhakika.
Sitta alisema serikali itatafuta mwekezaji atakayeingia ubia na
Tazara ambaye atapewa masharti ya kusafirisha mizigo itakayowezesha
kupata fedha za kulipa mishahara wafanyakazi.
"Msiendelee na tishio la migomo,dawa ipo jioni,serikali haiwezi
kuwatupa,itawalipa Haki zenu zote, jambo la msingi Tazara ifanye Kazi
kwa kushirikiana na taasisi nyingine,serikali itahakikisha Kabla ya
Oktoba Tazara itakuwa inakimbia na siyo kutembea,"alisema.
MABEHEWA MABOVU
Akiwa Kampuni ya Reli Nchini (TRL), Sitta alisema tume zote za
uchunguzi zilizoundwa na DK.Mwakyembe kuchunguza vigogo waliohusika na
kununua mabehewa mabovu hatazivunja badala yake zitaendelea na kazi kama
kawaida ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Dk.Mwakyembe akiwa katika Wizara ya Uchukuzi alidhibiti wizi mkubwa
uliokuwa ukifanywa katika taasisi na idara zilizopo chini ya wizara
hiyo hususani TPA ambako ilifikia wakati makontena ya mizigo ya wateja
ilikuwa ikiyeyuka katika mazingira yenye utata.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment