Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimemfikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe, Lucas Mweri, kwa madai ya kuvuruga uchaguzi wa serikali za
mitaa na kusababisha zaidi ya vijiji 80 kutofanya uchaguzi huo
uliyofanyika Desemba 14, mwaka jana.
Mweri ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo amefikishwa
kizimbani pamoja na wasimamizi wasaidizi wa vijiji na Kata za Wilaya
hiyo.
Katika madai yaliyowasilishwa na mwanasheria wa Chadema, Frederick
Kihwelo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe, A.J
Kirekiano ni kwamba wasimamizi hao walivuruga kwa makusudi uchaguzi huo
na kusababisha zaidi ya vijiji 80 kutofanya uchaguzi huo.
Chama hicho kinaeleza kuhujumiwa katika uchaguzi huo kwa wagombea
wakekuenguliwa dakika za mwisho bila kufuatwa kwa kanuni, taratibu na
sheria ya uchaguzi.
Hata hivyo kesi hiyo imeairishwa baada ya kutajwa na kupangiwa kusikilizwa Februari 18, mwaka huu.
Wakielezea sakata hilo baada ya kesi hiyo kuairishwa, Katibu wa
Chadema, jimbo la Korogwe Vijijini, Salum Sempoli, alisema vijiji 98 vya
jimbo hilo havikufanya uchaguzi baada ya wagombea wao kuenguliwa na
msimamizi wa uchaguzi.
Sempoli alieleza kuwa mkurugenzi huyo wa halmashauri akiwa
msimamizi wa uchaguzi aliwaengua visivyo halali wagombea wa nafasi za
uenyekiti wa vitongoji na vijiji sambamba na wajumbe bila sababu za
msingi.
إرسال تعليق