Kigogo wa TRA kashfa ya Escrow apata dhamana

Dar es Salaam.  Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa anayekabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh 1.6 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi, Frank Moshi jana alimuachia huru Mutabingwa baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha fedha taslimu Sh 1bilioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Mutabingwa aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kuwasilisha  hati tano za nyumba za watu mbalimbali  zenye thamani ya Sh 1.332 bilioni, wadhamini watatu ambao kati yao wawili walikuwa wafanyakazi wa TRA na mmoja mjasiliamari.
Kila mdhamini kati ya wadhamini hao,  kila mmoja alisaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh340 milioni na mshtakiwa huyo aruhusiwi kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu Moshi alimuachia huru mshtakiwa huyo na akaiahirisha kesi hadi Januari 29,2015 ambapo mshtakiwa huyo atasomewa maelezo ya awali (PH).
Awali akisomewa hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo alidaiwa kuwa  alitenda makosa ya kuomba na kupokea rushwa  kinyume na kifungu cha 15 (1)(a) cha sheria ya kupambana na rushwa  namba 11 ya mwaka 2007.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai akimsomea mashtaka hayo yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda kuwa  Januari 27, 2014 katika Benki ya Mkombozi  wilaya ya Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba 00110202613801.
Swai alidai  kuwa mshtakiwa huyo akiwa katika Benki ya Mkombozi alijipatia kiasi hicho cha fedha  ambacho ni  sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alizipokea kutoka kwa James Burchard Rugemalira  ambaye ni Mshauri huru wa Kitaalam, Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni ya  Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni mali  ya Rugemalira  mahakamani  kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Post a Comment

Previous Post Next Post