Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa (Nida), imesema
zoezi la kutoa vitambulisho vya uraia bado linaendelea jijini Dar es
Salaam na Zanzibar na kwamba hawana idadi rasmi ya ya wananchi ambao
wameshasajiriwa na kukabidhiwa vitambulisho vyao.
Hata hivyo, Nida imesema idadi hiyo huenda ikajulikana baada ya
kuanza kutumika kwa mfumo mpya unaotarajia kuanza karibuni wa kutoa
taarifa hizo kila baada ya miezi sita.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Nyaraka wa Nida, Thomas William,
alisema hawajapata idadi ya wananchi ambao wameshakamilishiwa
vitambulisho kutoka kwenye vituo vilivyoidhinishwa na mamlaka hiyo kwani
watu wengi bado wanaendelea kusajiriwa, kupigwa picha na kupokea
vitambulisho.
Alisema hivi karibuni Nida itaandaa utaratibu wa kutangaza taarifa
ya maendeleo ya zoezi hilo ikiwamo idadi ya wananchi ambao tayari
wamekabidhiwa vitambulisho kila baada ya miezi sita.
Kwa mujibu wa William, ugawaji wa vitambulisho pia unaendelea kwa
wakazi wa Zanzibar baada ya zoezi la usajiri kukamilika visiwani humo.
Alisema wananchi wanaendelea kukabidhiwa vitambulisho vyao baada ya
kupokea taarifa kwa kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno
kwa njia ya simu kisha kwenda kwenye vituo husika ambavyo vimetengwa na
Nida. Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inaendelea na usajiri kwa wakazi wa
mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Lindi na Mtwara huku mikoa ya
Kilimanjaro na Ruvuma ikiwa kwenye maandalizi ya zoezi hilo.
Alisema, maandalizi ni muhimu kufanyika kwanza kabla mamlaka hiyo
haijaanza rasmi usajiri wa wakazi wa eneo husika na badaye kupigwa picha
na kupewa vitambulisho.
Post a Comment