Nida: Hatuna idadi ya waliopata vitambulisho

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Nyaraka wa Nida, Thomas William.
Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa (Nida), imesema zoezi la kutoa vitambulisho vya uraia bado linaendelea jijini Dar es Salaam na Zanzibar na kwamba hawana idadi rasmi ya ya wananchi ambao wameshasajiriwa na kukabidhiwa vitambulisho vyao.
 
Hata hivyo, Nida imesema idadi hiyo huenda ikajulikana baada ya kuanza kutumika kwa mfumo mpya unaotarajia kuanza karibuni  wa kutoa taarifa hizo kila baada ya miezi sita.
 
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Nyaraka wa Nida, Thomas William, alisema hawajapata idadi ya wananchi  ambao wameshakamilishiwa vitambulisho kutoka kwenye vituo vilivyoidhinishwa na mamlaka hiyo kwani watu wengi bado wanaendelea kusajiriwa, kupigwa picha na kupokea vitambulisho.
 
Alisema hivi karibuni Nida itaandaa utaratibu wa kutangaza taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo ikiwamo idadi ya wananchi ambao tayari wamekabidhiwa vitambulisho kila baada ya miezi sita. 
 
Kwa mujibu wa William, ugawaji wa vitambulisho pia unaendelea kwa wakazi wa Zanzibar baada ya zoezi la usajiri kukamilika visiwani humo.
 
Alisema wananchi wanaendelea kukabidhiwa vitambulisho vyao baada ya kupokea taarifa kwa kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya simu kisha kwenda kwenye vituo husika ambavyo vimetengwa na Nida. Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inaendelea na usajiri kwa wakazi wa mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Lindi na Mtwara huku mikoa ya Kilimanjaro na Ruvuma ikiwa kwenye maandalizi ya zoezi hilo.
 
Alisema, maandalizi ni muhimu kufanyika kwanza kabla mamlaka hiyo haijaanza rasmi usajiri wa wakazi wa eneo husika na badaye kupigwa picha na kupewa vitambulisho.

Post a Comment

أحدث أقدم