Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa
Morogoro, Mary Moyo, shahidi huyo ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai ( RCO) wa mkoa wa Morogoro, Japhet Kibona, alidai kuwa
Agosti 9 , 2013, Polisi walipata taarifa za kiinterejensia kuwa Sheikh
Ponda angefika mkoani Morogoro kwa ajili ya kuhudhuria kongamano la Eid
pili, hivyo polisi iliwataka waandaji wa kongamano hilo kumsalimisha
polisi kiongozi huyo.
Kibona ambaye kwa sasa ni RCO wa mkoa wa Mtwara, alidai kuwa polisi
walitaka Sheikh Ponda ajisalimishe kwa sababu alikuwa akitafutwa
kutokana na tuhuma za kutoa maneno ya kashfa na uchochezi jijini Dar es
Salaam na Zanzibar.
Alidai kuwa Sheikh Ponda alikaidi amri hiyo ya kujisalimisha,
badala yake alifika mkoani Morogoro na kutoa maneno ya uchochezi dhidi
ya Waislamu na serikali huku akihusisha gesi iliyogunduliwa Mtwara na
mgogoro wa ardhi wa Loliondo pamoja na kamati za ulinzi na usalama za
kwenye misikiti na kuwataka Waislamu kufunga milango na madirisha kisha
kuwapiga watu wataojitambulisha kuwa ni kamati hizo kwenye misikiti.
Alisema baada ya Sheikh Ponda kutoa maneno hayo ambayo yaliumiza
imani za dini na kukiuka masharti ya kibali kilichotolewa na Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) na yeye kama RCO aliwapanga askari kwa
ajili ya kumkamata Ponda, lakini askari hao walishindwa kutokana na
wingi wa watu waliohudhuria kongamano hilo.
Alieleza kuwa katika harakati za kumkamata ghafla Sheikh Ponda
bahati mbaya aliigizwa ndani ya gari dogo na wafuasi wake na kumpeleka
kusikojulikana.
Kibona alidai kuwa baadaye alipata taarifa kupitia mitandao ya
kijamii kuwa Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi katika bega la mkono wa
kulia.
Aliongeza kuwa akiwa na maofisa wenzake walikwenda katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro, lakini Sheikh Ponda hakuwapo na
siku iliyofuata alipata taarifa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbiri.
Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro, alimuuliza shahidi huyo kuwa
nani alimpiga risasi Sheikh Ponda ikiwa polisi ndiyo walikuwa na silaha
za moto katika kongamano hilo na je anafahamu kuwa mmoja kati ya askari
waliokuwapo kwenye kongamano hilo alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi
wa tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda na je, kikosi hicho
kilishindwa nini kumkamata Sheikh Ponda ambaye hakuwa na silaha yoyote?
Kibona akijibu maswali hayo huku akiongozwa na wakili mkuu
mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola, alidai kuwa hafahamu kama kuna
askari aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi
kwa Sheikh Ponda na kwamba hawezi kufahamu nani aliyehusika kumpiga
risasi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 2 mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق